WAKATI dunia ikiamini kuwa janga la corona litapita na kuleta pambazuko jipya kwenye maisha litakaloturejesha katika tamaduni zetu za mwanzo kama tulivyozoea, lakini hali inazidi kuwa mbaya baada ya kuibuka kilio kingine kwa Watanzania.
Pamoja na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mamlaka pamoja na wataalamu wetu katika kutokomeza janga la corona, Watanzania ni kama wanajaribu kuvunjwa moyo kwa namna nyingine na kuyaona maisha yao yakizidi kuwa magumu kila kukicha tofauti na awali.
Ugumu huu unachangiwa na uhaba wa bidhaa ya sukari, ambayo hakuna haja ya kuficha maneno kusema kwamba ‘hakuna sukari’ kwenye maduka mbalimbali hatua inayowaumiza wananchi.
Kama hiyo haitoshi, ni kwamba hata ile kidogo iliyokuwa imesalia madukani bei yake nayo bado ilikuwa mtihani mwingine kwa wananchi hatua ambayo imesababisha baadhi ya familia kufuta kabisa utaratibu wa kupata kifungua kinywa huku baadhi wakihamia kutumia asali.
Katika hilo, mtihani mgumu na mzito unakuja kwa waamini wa dini ya Kiislam nchini, ambao wako kwenye kutimiza moja ya nguzo muhimu kwenye dini hiyo ambayo ni mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mwezi ambao sukari huitajika zaidi kushinda kipindi kingine chochote lakini ukakasi unasalia kuwa palepale kwamba ‘hakuna sukari.’
Pamoja na kwamba Serikali kuweka bei elekezi kufikia Sh 2,600 kwa jijini Dar es Salaam na Sh 3,200 kwa mikoa mingine, hatua hiyo ni kama haijawashtua baadhi ya wachuuzi wa bidhaa hiyo badala yake ni kama imeongeza ugumu zaidi.
Aprili 23 mwaka huu, Serikali ilitangaza ukomo wa kiwango cha juu cha bei ya sukari kwa rejareja kila mkoa na kusisitiza itachukua hatua kali kwa mfanyabiashara atakayebainika kuuza bei ya juu.
Bei hizo zilitangazwa wakati wa mkutano wa pamoja baina ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa kwa lengo la kukabaliana na changamoto ya kupanda kiholela kwa bei ambayo sasa imefikia wastani wa Sh 4,000 hadi 4,500 kwa kilo.
Akitangaza bei hizo, Hasunga anasema zimezingatia umbali wa kila eneo katika mikoa yote nchini na kuwataka wafanyabiashara kuzingatia maelekezo ya Serikali.
“Yeyote atakayekiuka maelekezo haya atakuwa ametenda kosa na hivyo atafikishwa katika vyombo vya sheria ili apate adhabu ambayo itahusisha ama kunyang’anywa leseni ya biashara, kulipa faini au adhabu zote kwa pamoja. Tutachukua hatua kali za kisheria kwa mfanyabiashara yeyote ambaye atakiuka masharti haya,’’ anasema Hasunga.
Anataja bei ya sukari kwa rejareja kwa kila mkoa kuwa ni Iringa (2,900), Mbeya (3,000), Rukwa (3,200), Katavi (3,200), Ruvuma (3,200), Njombe (2,900), Lindi (2,800), Mtwara (2,800), Arusha (2,700), Kilimanjaro (2,700), Manyara (2,700), Tanga (2,700), Dar es Salaam (2,600), Pwani (2,700) na Morogoro (2,700).
Mikoa mingine ni Kagera (3,000), Mwanza (2,900), Simiyu (2,900), Shinyanga (2,900), Geita (2,900), Mara (3,000), Kigoma (3,200), Singida (2,900), Tabora (2,900), Dodoma (2,900) na Songwe (3,000).
Jambo la kushtua ni kuwa bei hiyo elekezi ni kama ilichochea kabisa kutoweka kwa bidhaa hiyo kwenye maduka mengi huku wachache tu wakijaribu kufuata agizo hilo.
Kilichotokea hivi sasa ni kwamba uende dukani uambiwe hakuna sukari au ukubali kuinunua kwa Sh 3,200 hadi Sh 4,000 kwa kilo moja huku robo ikiuzwa Sh 800 hadi 1,000.
Lakini, pamoja na hayo hatari zaidi ni kwamba kati ya maduka 10 utakayotembelea kuulizia bidhaa hiyo kwa maeneo ya Dar es Salaam, ni maduka mawili hadi matatu tu utakayoambiwa kuwa bidhaa hiyo inapatikana.
Katika hili nalo kuna maswali mengine ya kujiulzia ambayo bado hayana majibu ya moja kwa moja.
Je, agizo la serikali la kuweka bei ya kikomo ndiyo umekuwa mwiba na kufanya baadhi ya wachuuzi kuachana na biashara hiyo kwa kuwa walitarajia kunufaika zaidi hususan katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani?
Au je, wameamua kuficha bidhaa hiyo muhimu baada ya kusikia taarifa za kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya wachuuzi wanaopandisha kiholela bei ya bidhaa hiyo kama tulivyoshuhudia katika mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam? Hakuna anayefahamu.
Rais Dk. John Magufuli akikagua sukari kabla ya kufungwa kwenye mifuko alipotembelea kiwanda cha sukari cha Kagera mwaka 2017.
Hivyo, kwasasa ukihitaji bidhaa hiyo kwa bei hiyo elekezi itakubidi ufunge safari na kwenda kwenye maduka makubwa kama Mliman City na baadhi ya maeneo ikiwamo Sinza – Dar es Salaam, swali la kujiuliza ni kwamba mkazi wa Chanika au Mbagala ataweza kufunga safari kwenda Mlimani City kununua sukari kwa Sh 2,600?
Hili ni jambo ambalo mamlaka husika zinapaswa kulifafanyia kazi kwa ajili ya kusaidia maisha ya waliowengi.
Tukiacha wenzetu waliofunga Ramadhani, tukumbuke wapo wagonjwa ambao sukari kwao ni jambo la muhimu zaidi ili kufanikisha afya zao na mahitaji mengine, kwani tumeshuhudia hata baahi ya migawaha kikombe cha chai kikipanda maradufu kile cha Sh 200 kikifika Sh 300 na kile cha Sh 500 kikifiakia 700 je, tunaelekea wapi huku.
Hali ya uzalishaji
Kwa mujibu wa Waziri Bashungwa, viwanda vinne vya ndani vilipanga kuzalisha tani 345,296 lakini zilizozalishwa ni tani 298,949.
Viwanda hivyo na kiasi cha tani kilichopanga kuzalisha na kile kilichozalishwa kwenye mabano ni Kilombero Sugar Co. Ltd (120,183 – 103,122), TPC Ltd (90,815 – 88,968), Mtibwa Sugar Estates Ltd (33,513 – 20,705) na Manyara Sugar Co. Ltd (5,785 – 7,750).
‘‘Kutokana na hali halisi ya uzalishaji wa ndani wa sukari kuwa pungufu ya malengo ya uzalishaji, Serikali ilifanya makadirio ya kiasi cha sukari ya kuziba pengo la uzalishaji na kutoa vibali kwa wazalishaji ili kuagiza kukidhi mahitaji.
“Hadi sasa sukari iliyoagizwa kuja kuziba pengo la uzalishaji takribani tani 10,710 imeshaingia nchini inaendelea kusambazwa katika mikoa yote,” anabainisha Bashungwa.
Kwa mujibu wa Waziri Bashungwa, Aprili 24, 28 na 30 walitegemea kupokea tani 13,500 za sukari ya kuziba pengo na kwamba wangeendelea kupokea kiasi kingine mwanzoni mwa mwezi huu.
Aidha, anabainisha kuwa kiasi chote cha sukari kilichopo nchini na kinachoendelea kupokelewa kinatosheleza mahitaji ya sukari nchini.
“Kwa taarifa hii, tuwaombe wananchi wote kuwa watulivu kwa sababu nchi yetu inayo sukari ya kutosha, Serikali haitakubali kuona wafanyabiashara wakipandisha bei kiholela.
“Wafanyabiashara wenye tabia hizi za kupandisha bei kiholela waache mara moja kwani Serikali haipo tayari kuona wananchi wake wanaumia kwa manufaa ya watu wachache,” anabaisha Bashungwa.
Mahitaji ya sukari nchini
Waziri Hasunga anabainisha kuwa mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida nchini yanakadiriwa kufikia tani 470,000 kwa mwaka na kwamba kiasi hicho ni kwa wastani wa mahitaji ya tani 38,000 kila mwezi pamoja na tani 14,000 za dharura.
Anafafanua zaidi kuwa uwezo wa viwanda vya ndani kwa msimu wa 2019/20 kulingana na makadirio ya mwanzoni mwa msimu yaani Julai, 2019 ni kuzalisha tani 378,000 za sukari ambacho ni sawa na asilimia 82.9 ya mahitaji halisi ya tani 456,000 ambayo hayajumuishi kiasi cha dharura cha tani 14,000.
“Uwezo huu wa uzalishaji wa viwanda vya ndani unaacha pengo la tani 78,000 ili kuweza kutosheleza mahitaji halisi ya tani 456,000 bila kiasi cha dharura cha tani 14,000.
“Hata hivyo, uwezo huu wa uzalishaji wa viwanda vya ndani ulitarajiwa kufikiwa pale tu panapokuwa na hali nzuri ya hewa na ufanisi mzuri wa viwanda,” anabainisha Hasunga.
Waziri huyo anataja changamoto ambazo zimeukumba msimu wa uzalishaji sukari wa mwaka 2019/2020 kuwa ni mvua nyingi kupita kiasi ambayo imesababisha uvunaji wa miwa kuwa mgumu, mlipuko wa magonjwa ya miwa kama vile viding’ata wa njano, uharibifu wa mitambo ya baadhi ya viwanda na kuchelewa kupatiwa vipuri.
Anakiri kuwa sababu hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa viwanda vya ndani kushindwa kufikia malengo ya kuzalisha tani 378,000 za sukari kwa msimu wa 2019/20.
Bodi ya Sukari
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, anabainisha kuwa sukari ipo ya kutosha isipokuwa kuna wafanyabiashara ambao si waadilifu wanaficha ili wauze kwa bei kubwa.
Aidha, Profesa Bengesi anasema kwasasa kuna operesheni inafanyika nchi nzima ya kuwakamata wafanyabiashara wanaoficha sukari na wengine wanaouza bei kubwa.
“Sukari ipo ya kutosha lakini kuna wafanyabiashara wachache ambao sio waadilifu wanaficha sukari kwa sababu ya corona na mwezi huu wa Ramadhani ili wauze kwa bei kubwa.
“Kutokana na hilo, hivi sasa kila mkoa kuna operesheni inayoendelea ya kuwakamata wafanyabiashara wanaofanya hivyo na tayari wengi wamekamatwa katika maeneo mengi. Zoezi hili linaongozwa na wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo yote,” anabainisha Profesa Bengesi.
Katika hili serikali na mamlaka zake hazina budi kufanyia kazi ili kuweza kuwasaidia Watanzania hawa wanaohangaika kwa kukosa sukari.
Pamoja na kwamba Serikali ilitoa bei hiyo elekezi katika Mkoa wa Dar es Salaam kuwa kilo moja ni Sh 2,600 lakini baadhi ya maduka mambo yamekuwa ni tofauti badala yake ikitokea umebahatika basi utainunua kwa Sh 2,800.
Nakumbuka kuwa hata mara ya mwisho bei ya sukari kupanda mazingira yake yalikuwa yakifanana fika na haya badala yake bei ikabakia kuwa hiyohiyo hadi leo, hivyo ni wakati kwa serikali kutilia mkazo zaidi katika hili.