Tanasha Soma Hiyo Kutoka Kwa Wema, Mobeto!


MAUMIVU mengine hupotea baada ya siku kadhaa. Mengine wiki au miezi kadhaa. Mengine huchukua miaka kupotea na kuna mengine hayapotei kabisa, yananabaki siku zote hadi mtu unapelekwa kaburini, jambo ambalo vitabu vitakatifu vinakataza.

Kwa kawaida baada ya maumivu ya kidonda kinachobaki ni kovu. Kovu ni kumbukumbu tu, lakini isiyo na maumivu. Kuna sababu nyingi zinazoleta vidonda vinavyoacha makovu. Kuna makovu yanayoachwa na vidonda vilivyopatikana katika kujifunza vitu kama vile wakati wa utoto unapojifunza kutembea ukaanguka na kuumia.

Bila kujifunza huwezi kufahamu na katika kujifunza unakutana na maumivu na vidonda vinavyoacha makovu.

Vidonda vya makovu haya yote vinauma, lakini kuna ambavyo maumivu yanaishia mwilini na mengine yanaingia hadi rohoni, katika maisha yetu ya kawaida pia tunakutana na kuumia kwingi, kunakoacha maumivu kisha vidonda, halafu makovu ya aina mbalimbali.

Makovu mengine unayasahau baada ya muda mfupi, lakini mengine yanang’ang’ania. Unaweza kuumizwa kwenye uhusiano wako kwa kuachwa au kuachana na mtu uliyempenda, hali ikawa mbaya mno kiasi cha kukosa sababu ya kuendelea kuishi, lakini unapopata mwingine unasahau yote. Unasahau kama uliwahi kuumizwa moyoni mwako. Unakuwa huna tena kovu ndani yako!

Pamoja na hayo, lakini maumivu ya kutendwa na mpenzi, mchumba, mke au mume uliyempa moyo wako wote na kuamini ndiye utakayesafiri naye kwenye maisha yenu hadi kifo kiwatenganishe, mara nyingi hukaa muda mrefu au hayaishi kabisa.

Katika haya yote unapaswa kujua kuwa kovu halina maumivu. Litakuwepo pale kukukumbusha tu kuwa ulipitia haya na sasa umevuka. Litakuwepo pale kukuonya kuwa usipite mahali fulani utaumia na kukutia moyo kuwa yamepita na sasa ni mshindi na kwa imani tunasema umeshinda na zaidi ya kushinda.

Hicho ndicho anachopaswa kukijua mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna.

Tanasha anapita kwenye maumivu makali baada ya kudai kutendwa na Diamond au Mondi aliyezaa naye mtoto mmoja wa kiume, Naseeb JR. Tanasha aliamini hapo ndipo moyo wake utakapotulia. Kumbuka ukijiaminisha kupata kitu fulani, halafu ukakikosa, moyo huumia mno!

Lakini pamoja na hayo yote, Tanasha ana kitu cha kujifunza kwa wapenzi wengine wa zamani wa Mondi kama Wema Isaac Sepetu na Hamisa Mobeto.

Pamoja na kwamba mwanzoni walikuwa maadui baada ya wote kutembea na Mondi na kuachwa solemba, lakini sasa ni marafiki wakubwa, wamesahau yaliyopita ambayo si ndwele, badala yake wanaganga yajayo.

Wema na Mobeto wanakuwa ni ushuhuda kwamba, kutoka kimapenzi na mwanaume mmoja si uadui kwa kuwa kila mmoja alikuwa na mpenzi huyo kwa wakati wake.

Kubaini kwamba mtu amekuchukulia mwenza wako, haina maana kuwa ndiyo mwanzo wa vita kuu ya tatu ya dunia.

Wema na Mobeto sasa ni mashosti wakubwa. Wanajaliana kwa hili na lile, upendo umetawala ndani yao.

Ilianza kidogokidogo. Mobeto alianza kuufungua moyo wake na kumpongeza Wema kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa anapendeza, jambo ambalo liliwafanya baadhi ya mashabiki wao kupigwa na butwaa.

“Wema umependeza sana… anything for you my love….” aliandika Mobeto na kusababisha gumzo kama lote kwani wawili hawa walijulikana kama mahasimu wakubwa.


Kwa mujibu wa mashabiki wao, Wema na Mobeto sasa wamekua, wanakubaliana na ule usemi usemao; ‘hakuna adui wa kudumu kwenye maisha ya mwanadamu!’

Ukweli ni kwamba, Tanasha ana somo la kuchukua kutoka kwa Wema na Mobeto. Hana sababu ya kuendelea kuwa mkali kwa kila mtu hasa mwenye ukaribu na Mondi na familia yake. Inafahamika, pamoja na kwamba, si wapenzi wake kwa sasa, lakini Wema na Mobeto ni marafiki wakubwa wa Mondi na familia yake.

Unajua kwa nini? Wema na Mobeto wamekubali yaishe, wameamua kusonga mbele pamoja na kwamba wamekosa fursa muhimu ya kuolewa na Mondi.

Katika makala hii, nimezungumza na Tanasha ambaye tangu atengane na Mondi mapema mwaka huu, ameshindwa kusonga mbele, badala yake anatoa tu maneno makali ya kukashfu familia ya jamaa huyo.

Najua mtaniuliza vipi kuhusu Zari? Huyu makala yake inakuja, usikose kufuatilia gazeti hili.

MAKALA: NEEMA ADRIAN, BONGO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad