ALIYEWAHI kuwa mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elisa Mollel, ambae hivi karibuni alitaganza nia yake ya kutaka kurudi tena kugombea ubunge amefariki dunia ghafla jana alfajiri.
Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Arumeru, Charles Beda, amesema kuwa enzi za uhai wake Mollel alikuwa ni mtu wa watu na hakuwa na makuu, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Pamoja na kifo hicho cha Molell bado alisema familia hiyo imekutwa na misiba mfululizo ambapo hivi karibuni ilimpoteza kijana wake ambaye alikuwa akitajwa kuwania ubunge.
“Kwa niaba ya CCM napenda kutoa pole nyingi sana kwa familia kutokana na msiba huu mkubwa na taarifa zaidi familia itazitoa,” amesema Beda.
Mei 18 mwaka huu (2020), Mollel alitangaza uamuzi wa kugombea jimbo hilo pindi muda utakapowadia kwa kuwa ana uzoefu mkubwa na siasa za jimbo hilo.
Mbali na kauli hiyo Mollel alisema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akifuatwa na makundi ya watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa mila maarufu kama Malaigwanani, viongozi wa dini na kina mama wakimshawishi agombee ubunge mwaka huu.
Hadi sasa makada mbalimbali kupitia CCM wilayani Arumeru Magharibi wametangaza nia, nao ni Mathias Manga, Robinson Meitinyiku, Thomas Ole Sabaya na mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Goodluck Ole Medeye.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibni jijini Arusha, Mollel alisema kuwa tangu alipong’atuka katika utumishi wake baadhi ya wananchi wilayani humo wamekuwa wakimfuata na kumtaka achukue fomu kwa madai mambo hayaendi sawa.
“Wananchi wananifuata na kuniambia mambo ni hovyo tangu nilipoondoka, nimefuatwa na makundi mengi tu na mimi nasema muda ukifika nitasema jambo,” alisema Mollel.
Hata hivyo, alisisitiza ya kwamba tangu ang’atuke miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimsikitisha ni pamoja na ubovu wa miundombinu, kero ya maji sanjari na kero ya migogoro ya ardhi, matatizo aliyodai yameshindwa kutatuliwa na mrithi wake.
Aidha, alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo anajivunia hadi sasa ni pamoja na rekodi yake ya kuboresha sekta ya elimu wilayani humo ambapo aliondoka huku akiwa amefanikiwa kuacha shule za sekondari 26 tofauti na alipoingia madarakani.
“Hapo awali tulikuwa na watoto wengi sana wanamaliza elimu ya msingi lakini hawaendi sekondari; nimeondoka na kuacha shule za sekondari 26 katika kila kata, najivunia kwa hili,” alisema Mollel.