Kama taifa, Mungu alitupendelea sana kutupa vichwa ambavyo vilifanya poa sana kwenye muziki wa Hip Hop Bongo. Lakini kwa mipango yake Mungu, wapo marapa ambao waliweka alama kubwa sana kwenye muziki wa Hip Hop Bongo kisha wakafariki dunia, Mungu awalaze mahali pema peponi, amina. Licha ya kutangulia mbele za haki, leo tuwaangalie marapa watano waliotokea kwenye ardhi hii ya Nyerere na kuweka alama ambapo mchango wao utakumbukwa vizazi na vizazi:
MTOTO WA DANDU
Huyu yeye alifariki miaka mingi iliyopita. Ni miongoni mwa marapa waliokuwa wa kwanza kwanza kwenye Bongo Fleva kipindi ambacho muziki wa Bongo Fleva ulikuwa bado haujashika hatamu lakini kazi zake nzuri alizotoa zinaishi mpaka sasa.
Miongoni mwa ngoma zake kali ni pamoja na Sina Makosa, Mpenzi alioshirikiana na Mary G na nyingine nyingi.
Alifariki kwa ajali ya gari na huyu ndiye aliyekuwa muasisi wa Tuzo za Kilimanjaro Music.
MANGWAIR
Albert Mangwair, ni moja kati ya marapa bora kuwahi kutokea Bongo Land, ni msanii ambaye alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuchana mashairi ya papo kwa papo. Moja kati ya ngoma zilizowahi kuacha alama kutoka kwenye library yake ni pamoja na Mikasi (shukrani sana kwa P Funk aliyepiga biti bora la miaka yote).
Kama hiyo haitoshi, Ngwair ameacha alama kwa nyimbo nyingine kali kama She Got A Gwan, Nipe Dili, Dakika Moja, Spidi 120 na CNN. Niamini, ingia YouTube zisikilize hizi nyimbo sasa hivi halafu utaniambia nini maana ya msanii.
Huyu yeye alipatwa na mauti huko Sauz huku ikielezwa kifo chake kilitokana na kuzidisha kilevi.
LANGA
Langa Kileo ni moja kati ya marapa ambao walikuwa wa tofauti sana. Walitoa mchango mkubwa sana kwenye gemu. Aliingiza mistari hatari sana kwenye moja kati ya kolabo bora kuwahi kutokea kwenye hii dunia ambayo ni wimbo wa Ni Hayo Tu.
Kenye ngoma hiyo ambayo pia alishirikishwa na Profesa Jay, Langa alichana hivi: “Natumia akili, ustarabu na subira, situmii mwili jazba na hasira, mapinduzi daima, misimamo kama Che Guevara…”
Jamaa aliacha alama kwa ngoma zake kali kama Matawi ya Juu, Gangster, Rafiki wa Kweli, Pipi ya Kijiti na nyingine kibao.
GEEZ MABOVU
Geez Mabovu ni rapa ambaye ameacha rekodi yake ndani ya muziki wa Hip Hop Bongo. Mtoto wa Kiume ni miongoni mwa ngoma yake ambayo inaishi miaka nenda rudi, niamini mimi. Isikilize hata leo hii halafu utaelewa ninachomaanisha.
Achana na hiyo, kuna Dakika Sifuri. Hili biti lilikuwa matata sana. Mpishi wake alikuwa Lamar ambaye kwa sasa hasikiki sana kwenye gemu lakini ni hatari. Nikumegee siri kidogo, chukua muda wako leo hii halafu sikiliza wimbo wa Nilikotoka aliomshirikisha Joh Makini, utakubaliana na mimi kwamba Mungu alitupendelea sana kuwa na hiki kichwa kwenye gemu.
GODZILLA
Alikuwa staa wa Hip Hop wa kizazi cha kati ndani ya Bongo. Staili yake aliyotoka nayo ilikuwa kama ya kumuiga staa wa Marekani Jay Z lakini asikwambie mtu, ameacha alama kwa ngoma kali kama vile get High, King Zilla aliomshirikisha Marco Chali.
Kama hiyo haitoshi, huyu mwamba ameacha alama pia kwenye ngoma nyingine kama Salasala na Nataka Mkwanja.
MAKALA:
Erick Evarist, Risasi