APRILI 13, siku nne tu tangu msanii Zuchu atambulishwe kuwa amesainiwa katika lebo ya muziki ya WCB ya Diamond Platnumz, tayari alikuwa na ujumbe mzito wake kuwashukuru mashabiki.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Zuchu aliandika ujumbe kwa lugha ya Kiingereza unaomaanisha: “Asanteni mashabiki wangu wapendwa kwa kuifanya EP yangu kuwa kwenye trending. Fikiria imeachiwa saa kadhaa tu zilizopita.”
Ulikuwa ni ujumbe muhimu wa shukrani kwa mafanikio ya haraka, mapokezi makubwa ambayo msanii yeyote mpya duniani angeyaomba. Lakini kama unavyoijua Insta. Haikuachi salama. Haikuachi hivi hivi. Mfuasi mmoja wa mtandao huo akaandika chini ya posti hiyo ya Zuchu: “Mashabiki wako? Sikufahamu kama nawe pia una mashabiki wako.”
Lilikuwa ni dongo zito kwa Zuchu. Yaani siku nne tu tangu atambulishwe tayari alikuwa na mashabiki wake!? Wapi? Hakuna aliyekuwa akimfahamu Zuchu kabla ya kutambulishwa na Wasafi.
Ingewezekanaje ndani ya siku nne tu ya kuachia EP ya nyimbo zake tayari awe ameshapanda kwenye chati ya trending? Ingewezekanaje kupata watu wengi hivyo wa kufuatilia kazi zake hadi aongoze kwenye trending?
Awali, siku moja tu tangu kuachia video ya wimbo wake wa ‘Wana’, tayari Zuchu alipata views laki 5. Na ndani ya siku mbili, alishapiga views milioni moja za wimbo huo na kushika namba 2 kwenye trending ya YouTube.
Kufikia sasa, video ya ‘Wana’ ina views milioni 2.9 inakimbilia milioni 3, mwezi mmoja tu tangu iachiwe. Hili si jambo la kulichukulia poa kwa sababu hata wasanii wakubwa wanahaha kupata views za kutosha. Rich Mavoko kwa mfano, memba wa zamani wa Wasafi, video ya wimbo wake wa ‘Sheri’ alioshirikiana na rapa Fid Q, ambayo ilitoka tangu 2017, hadi leo ina views milioni 2.6. Views laki tatu pungufu ya views za video ya Zuchu.
Mwezi mmoja tu tangu atambulishwe, Zuchu tayari ana wafuasi 338,000 kwenye akaunti yake ya Instagram. Ndio sababu akasema “Shukrani kwa mashabiki wangu wapendwa.”
Lakini kufuatiliwa kwa ukubwa huu wa mapema, hata bosi wake, Diamond mwenyewe hakuwahi kuupata wakati akiibuka. Alihangaika sana kwa miaka mingi, akirekodi hadi nyimbo akirap, ikiwamo ‘Jisachi’ aliowashirikisha Mangwair na Geezy Mabovu (wote sasa marehemu). Hakutoboa kirahisi Mondi.
Iko hivyo pia kwa msanii mpya, Ibraah, aliyesajiliwa katika lebo ya Konde Music Worldwide ambayo wengi wanaitambua kama Konde Gang ya Harmonize.
Ibraah ameachia EP yake ikiwa na ngoma kadhaa.
Wimbo wake wa kwanza chini ya Konde Gang uitwao ‘Nimekubali’, una views 612,000 wiki tatu tu tangu kuachiwa. Na ‘Sawa’ aliomshirikisha Harmonize una views 350,000 ndani ya wiki mbili tu. Haya si mafanikio madogo kwa msanii mpya ambaye ndio kwanza anaanza kusaka mashabiki wake.
Ni mafanikio ambayo kwa asilimia 99 yanatokana na umaarufu wa mabosi wao, Diamond kwa Zuchu na Harmonize kwa Ibraah.
Isingekuwa rahisi kwao kutoboa haraka hivi, achana na mahangaiko waliyopitia miaka ya nyuma kabla ya kuonwa, kuaminiwa na kutambulishwa kwenye lebo hizi maarufu nchini. Mashabiki watawapima kwa kile walichofanya baada ya kutambulishwa kwa sababu hapo kabla hawakuwa wakifahamika. Ndiyo maana mfuasi yule wa Insta akamhoji Zuchu: “Mashabiki wako? Sikufahamu kama nawe pia una mashabiki.”
Ni ngumu msanii mpya ndani ya siku nne tu tangu kutambulishwa awe na mashabiki wake. Hawa ni mashabiki wa Diamond na Harmonize ambao wanataka kuona wasanii wao wameleta vitu gani mezani.
Lile si swali baya wala la chuki. Ni swali linalowataka kutambua uhalisia uliowazunguka kwa sasa. Kila wanachofanya sasa kinafuatiliwa na mashabiki wa mabosi wao.
Ni wakati wao sasa watuonyeshe uwezo wao. Kisha wawe na mashabiki wao.
Zuchu anajua kiukweli
ReplyDelete