Takwimu za kitaifa za viashiria vya malaria kwa mwaka 2017 (Malaria Indicator Survey) inaonesha kuwa upatikanaji wa vyandarua (access) kwa wananchi kitaifa ni asilimia 63 na matumizi ya vyandarua kwa wanajamii kitaifa ni asilimia 52.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vyandarua kwa kila kaya uliofanyika wilayani Chunya.
Waziri Ummy amesema kuwa Mkoa wa Mbeya, upatikanaji wa vyandarua ni asilimia 62 na kiwango cha matumizi ya vyandarua kwa Mkoa ni asilimia 32 tu.
“Nchi yetu imepiga hatua kubwa na kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya Malaria ambapo kiwango cha maambukizi kimepungua kwa karibu asilimia 50, kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema hiyo ni kutokana na takwimu za matokeo ya utafiti wa viashiria vya Malaria katika jamii (MIS 2017) ambapo visa vipya vya Malaria vimepungua kwa asilimia 19 kutoka visa 150 kati ya watu 1000(2015) hadi visa 122 kati ya watu 1000(2019).
Ameongeza kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria vimepungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 6311 mwaka 2015 hadi vifo 2079 mwaka 2019.
“Kwa mkoa wa Mbeya pia maambukizi yapo kwa kiasi cha asilimia 4 kiwango hiki ni kidogo ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa asilimia 7.3.
Aidha, Waziri Ummy amesema kila mwanafamilia mwenye dalili za Malaria ahakikishe kuwa anawahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili kupimwa kabla ya kutumia dawa kwani sio kila homa ni Malaria na endapo atagundulika kuwa na vimelea vya malaria ahakikishe anatumia dawa kulingana na maelekezo ya mtoa huduma za afya na kumaliza dozi ili kuepuka usugu wa dawa mwilini.
Ugawaji wa vyandarua unafanyika kwa awamu tatu kupitia Bohari Kuu ya Dawa(MSD) ambapo awamu ya kwanza inajumuisha mikoa ya Mbeya,Songwe,Njombe na Rukwa
Awamu ya pili ni mikoa ya Iringa, Dodoma na Singida na awamu ya tatu na ya mwisho itahusisha mikoa ya Tanga,Kilimanjaro na Manyara.
Hata hivyo mikoa mingine iliyobaki itaendelea kupata vyandarua kupitia kliniki ya afya ya uzazi (wajawazito) na watoto chini ya mwaka mmoja na pia kupitia wanafunzi wa shule za msingi.