Kamishna wa Haki za Binaadamu, katika Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amelaani kifo cha Mmarekani mweusi, George Floyd kilichotokea mikononi mwa polisi, na kutaka serikali ya taifa hilo kudhibiti mauwaji ya Wamarekani, wenye asili ya Afrika wasio na silaha.
Katika taarifa yake kwa umma kiongozi huyo amesema hicho ni kisa cha hivi karibuni kabisa miongoni mwa mauwaji mengi ya jamii hiyo ya raia wasio na silaha. Aidha kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa alitaja majina kama ya Ahmaud Arbery na Trayvon Martin ambao pia waliuwawa.
Mfanyakazi wa mgahawani, George Floyd aliyekuwa na umri wa miaka 46 aliuwawa Jumatatu wakati akiwa katika mikono ya polisi huko katika mji wa kaskazini wa Minneapolis, na kuzusha maandamano ya wenye hasira katika maeneo mbalimbali.
Gadhabu za maandamano hayo zilichochewa zaidi na video iliyorikodiwa na mpita njia ikionesha polisi mzungu akitumia goti kumkandamiza shingoni Floyd aliyefungwa pingu huku akiomba msaada kutokana na kukosa pumzi.