Usiseme ‘hatuna pesa, sema sina pesa!’ Anachokifanya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ kwenye nyakati hizi kinadhihirisha kauli hiyo kwani staa huyo anaonesha jeuri ya pesa si ya nchi hii, Gazeti la IJUMAA limekukusanyia habari mpya inayomhusu
ISHU ILIVYOKUWA
Awali, katika mitandao ya kijamii, zilisambaa tetesi kuwa Mondi hana nyumba aliyojenga mwenyewe, licha ya ukubwa wa jina alilonalo na kuongeza kuwa, kazi yake ni kununua magari na kuyapaki kwenye nyumba za kupanga.“Yaani Mondi ni kama hana nyumba.
Ananunua tu magari ya kifahari, lakini yeye anaishi kwenye nyumba za kupanga,” aliandika mdaku mmoja kwenye ukurasa wa Instagram.
AIBUKA KUJITETEA
Baada ya muda, staa huyo mkubwa barani Afrika aliibuka na kukiri katika mahojiano na media yake, kwa kusema ni kweli nyumba anayoishi kwa sasa maeneo ya Mbezi-Chini jijini Dar amepanga, lakini ana nyumba yake ambayo anaijenga hivyo ikikamilika atahamia huko.
“Nakiri kweli nyumba ninayoishi kwa sasa Mbezi nimepanga, lakini ipo nyumba yangu ambayo ninaijenga, sema dream house yangu (nyumba ya ndoto yangu) ina vitu vingi ndani yake, ina sehemu ya basketball, sehemu ya kuangalia movie, yaani ni kubwa. “Nyumba yenyewe ipo Kigamboni, hivyo nasubiri ikamilike kisha nitahamia,” alisema Mondi alipokuwa akihojiwa kwenye vyombo vyake vya habari, Wasafi FM na Wasafi TV.
IJUMAA MZIGONI
Baada ya kusambaa kwa habari hizo na yeye mwenyewe kukiri, Gazeti la IJUMAA liliingia mzigoni, kuanza kuusaka mjengo huo maeneo ya Kigamboni.Kwa kuwa Kigamboni ni kubwa, IJUMAA lililazimika kufanya uchunguzi wake na kufanikiwa kulipata eneo husika kupitia vyanzo mbalimbali.
NI MIKWAMBE…Gazeti la IJUMAA lilipofika Feri-Kigamboni, lilifunga safari hadi Mikwambe na kukuta si tu kwamba ni nyumba anajenga, bali amenunua mtaa mzima kwa ajili ya kuweka makazi yake na vitu vingine.Unapofika kwenye eneo hilo, kuna geti kubwa ambalo unaingia kisha unakata kulia kuelekea kwenye hilo eneo la Mondi.
NYUMBA KAMA ZOTEIJUMAA
lilishuhudia kufuru si ya kitoto, kuna nyumba ambazo Mondi anajenga na nyingne zimekamilika.Kuna ambazo zimejengwa kwa mfumo wa kufanana kama ‘kota’, lakini pia kuna bonge la eneo ambalo lipo wazi ambapo kuna uwezekano wa kujenga viwanja vya basketbal au mabwawa ya kuogelea (swimming).
JIRANI AFUNGUKA
Gazeti la IJUMAA lilizungumza na mmoja wa majirani wa Mondi ambaye alieleza kuwa, lengo la jamaa huyo kununua mtaa huo ni kuweka makazi yake, lakini pia vitu vyake mbalimbali vya kufanyia muziki.“Yaani anataka hapa pawe ndiyo kila kitu kuanzia studio, makazi ya kruu yake yote, viwanja vya mazoezi na mambo mengine mengi,” alisema jirani huyo aliyeomba hifadhi ya jina.
GHARAMA SI YA KITOTO
Jirani huyo alisema kuwa, eneo hilo alikuwa analifahamu kabla na kwamba thamani yake inacheza kwenye shilingi bilioni mbili za Kibongo hadi tatu.“Yaani hapa itatengemea sasa Mondi kazungumza vipi na mwenye eneo, lakini linacheza kwenye bilioni mbili mpaka tatu,” alisema jirani huyo.Hata hivyo, alipokuwa anahojiwa Mondi, hakutaka kuweka wazi gharama halisi ya eneo hilo.
MLINZI AFUNGUKA
Awali, IJUMAA lilizungumza na mmoja wa walinzi wa eneo hilo ambaye alikuwa mgumu kuzungumza, lakini baada ya kushawishiwa alikubali na kutoa ushirikiano. Alisema, eneo hilo lote ni la Mondi na wiki tatu zilizopita alifika kuangalia maendeleo ya nyumba hizo kwani ziko katika hatua ya matengenezo.
“Ni kweli mwanamuziki Diamond amenunua nyumba katika eneo hili na haujapita muda mrefu ni wiki tatu hivi alifika hapa kuangalia maendeleo ya nyumba zake, kwa sababu ziko katika hatua ya matengenezo, bado hazijamalizika kujengwa,’’ alisema mlinzi huyo.
MAJIRANI WAFURAHIAIJUMAA
lilizungumza na baadhi ya madereva bodaboda wa eneo hilo ambapo walifunguka kwamba, wamefurahi kwani kwa sasa wanamuona ‘live’ Mondi.
“Ni kweli Mondi kanunua eneo hili, mara kadhaa nimekuwa nikimuona anafika kuangalia, mimi nimefurahi sana, kwa sababu huwa namuona kwenye TV ila sasa hivi nitakuwa ninamuona laivu kwa sababu yeye ni mtu poa sana,’’ alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hamisi.
MONDI SI WA MCHEZO
Hii ni kufuru nyingine kwa Mondi ndani ya muda mfupi katika kipindi hiki ambacho watu wengi wanalia njaa kutokana na janga la Corona. Hivi karibuni ametoka kutangaza kununua ghorofa (hoteli) maeneo ya Mikocheni B jijini Dar, lakini kama hiyo haitoshi, amevuta mkoko wa kifahari aina ya Rolls-Royce ambao thamani yake si chini ya shilingi milioni 800 za Madafu.