Wakili "Idris Sultan Anahojiwa Kwa 'Kuicheka Picha ya Rais Magufuli'
0
May 21, 2020
Wakili wa mchekeshaji maarufu nchini Tanzania Idriss Sultan ameiambia BBC kuwa msanii huyo anahojiwa na polisi juu ya 'kuicheka picha ya Rais John Pombe Magufuli'.
Kwa mujibu wa wakili Benedict Ishabakaki, japo bwana Sultan hajafunguliwa mashtaka rasmi na polisi, maswali anayohojiwa kufikia sasa yanahusiana na mkanda wa video aliotuma mitandaoni hivi karibuni akionekana akiicheka picha ya zamani ya rais Magufuli.
"Hawajamwambia mpaka sasa kama amevunja kifungu chochote cha sheria...lakini mwenendo wao wa maswali ni kuhusiana na ile video," wakili Ishabakaki ameiambia BBC.
Bw Sultan anashikiliwa na polisi toka Jumanne mchana punde tu alipoitikia wito wa kuripoti kituo cha polisi na mpaka sasa bado hajapatiwa dhamana wala kupandishwa kizimbani.
Wakili wake pia ameiambia BBC kuwa Jumatano jioni polisi walienda kufanya upekuzi nyumbani kwa mteja wake.
"Tunataraji anaweza kuachiwa kwa dhamana hii leo...masharti tuliyopewa ni awe na wadhamini wawili wanaotambuliwa na serikali ya mtaa," amesema wakili Ishabakaki.
Kumekuwa na kampeni katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania ambapo watu kadhaa wakiwemo wanasiasa wa upinzani wa wanaharakati wanatuma ujumbe wa kutaka msanii huyo kuachiwa huru.