Madaktari wameonya kuwa wanawake wengi wako katika hatari ya kupata saratani ya kizazi na utasa kutokana na kutumia sababu na kujipaka mafuta katika sehemu zao za siri.
Mshauri wa masuala ya uzazi kutoka nchini Kenya, Dkt Ramadhan Marjan, alisema mtindo wa wanawake kujipaka dawa za kukaza misuli ya uke umeenea sana nchini.
Alisema wanawake wengi wakiwemo walio katika ndoa, wameingilia uraibu huo wa kujipaka mafuta ya kukausha sehemu za siri wakiamini watafurahisha wapenzi wao, bila kujua madhara yanayotokana na tabia hiyo.
Dkt Marjan aliwashauri wanawake wasiwe na haja ya kutaka kukaza misuli, kwa kuwa sehemu hizo za kike zina uwezo wa kupanuka na kurejelea hali ya awali.
“Mafuta haya yanapotengezwa, watengezaji hawazingatii usafi wa mazingira. Bidhaa wanazotumia pia hazijulikani. Kuzitumia humweka mwanamke katika hatari ya kupata maambukizi katika kizazi, ambayo yasipotibiwa husababisha mwanamke kuwa tasa na kuugua saratani ya kizazi,” akasema.
Alieleza kuwa dawa hizo huharibu hali ya kawaida ya sehemu hiyo, na kumfanya mwanamke kuwa mkavu sana ukeni, hali inayosababisha kuchubuka wakati wa tendo la ndoa. Uchubukaji huo humweka katika hatari ya kupata maambukizi ya maradhi hatari kama vile Ukimwi miongoni mwa mengine ya zinaa.
“Kama misuli imekazana na hakuna mtelezo, hii humsababishia mwanamke maumivu makali na hata kupata vidonda wakati wa ngono au kujifungua,” alisema.
Aliwashauri wanawake waepuke matumizi ya bidhaa yoyote katika sehemu za siri, isipokuwa walizoandikiwa na daktari.
Chanzo: Taifa Leo, Kenya