NAHOD HA wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Victor Wanyama ameibuka na kumjibu beki wa kushoto Aboud Omar , ambaye hivi karibuni alitoa lawama kwa mchezaji huyo kuwa ndiye anayesababisha kuchelewa kulipwa kwa posho zao za Afcon 2019.
Wachezaji na benchi la ufundi, bado hawajalipwa kiasi cha Ksh 250,000 (ambazo ni sawa na Sh milioni 5.4 zilizoahidiwa kwa kila mmoja wao endapo watashinda mchezo wowote katika mashindano hayo nchini Misri.
Harambee Stars ilifanikiwa kuifunga timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, lakini sasa ni karibu mwaka mmoja umepita, bonasi hiyo bado haijatolewa kwa mchezaji yeyote aliyekuwemo katika kikosi hicho.
Katika mahojiano na Madgoat TV, Aboud, ambaye kwa sasa hana timu, alidai kuwa Wanyama alifanya makubaliano ya bonasi hiyo na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), lakini alishindwa kufuatilia vizuri.
Pia alisema Wanyama alishindwa kabisa kufuatilia suala hilo vizuri. Hatahivyo, Wanyama amejibu mapigo kwa kumtaka Aboud kuheshimu wachezaji wenzake wa timu hiyo ya taifa. Nafikiri kile alichosema (Aboud) kuhusu mimi ni kutoniheshimu na hakina ukweli wowote.
Nimejadiliana kila kitu na wachezaji na kila tulichokubaliana na Shirikisho. Na sasa ni nafasi ya FKF kutimiza ahadi waliyoitoa, “alisema Wanyama.
“Ukweli ni suala na ile Sh milioni 50 (sawa na Sh bilioni 1 za Tanzania zilizotolewa kwa timu hiyo na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto. FKF walitaka wapate sehemu kubwa ya fedha hizo wakidai kuwa ni sehemu ya bajeti yao ya Afcon 2019. Niliweza kukubaliana na FKF na yote haya yalifanyika katika majadiiano kupitia uongozi wa wachezaji, “alisema Wanyama.
MFADHAIKO “Huwezi kunipenda mimi, unanichukia mimi kama mtu binafsi, lakini nipatie mimi na wachezaji wengine heshima tunayostahili. Kama mchezaji wa kulipwa kila kitu mnachozungumza katika vyumba vya kubadilishia nguo kilatakiwa kubaki kule kule… ,“aliongeza Wanyama.
Wanyama pia alisisitiza umoja miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa akisema hilo ni muhimu katika kupambania haki zao na kuendelea hata kama ni kwa mtu binafsi.