Wataalamu ni Chukizo Kubwa Kwa Wanasiasa..Ona Kilichomtokea Huyu Daktari Aliyegundua Uwepo wa Ugonjwa wa Corona
0
May 07, 2020
FEBRUARI 7, mwaka huu, China ilimpoteza daktari bingwa, jina lake ni Li Wenliang. Alikuwa kijana mdogo. Oktoba 12, mwaka huu, angetimiza umri wa miaka 34.
Wenliang alikuwa anahudumu kwenye Hospitali Kuu ya Jiji la Wuhan. Desemba mwaka jana, alikuwa mtu wa kwanza kuushitukia mlipuko wa ugonjwa mpya unaosababishwa na virusi hatari.
Kuhakikisha anaokoa wenzake, Wenliang aliwajulisha wafanyakazi wenzake 30 kwa njia ya mtandao wawe makini na wagonjwa wapya, maana ilionekana wana alama na dalili zenye kushabihiana na homa ya SARS, iliyoua watu 774 barani Asia kati ya mwaka 2002 na 2004.
Tahadhari hiyo ya Wenliang kwa wafanyakazi wenzake wa Hospitali Kuu ya Wuhan, ilivuja mpaka kwenye mitandao ya umma. Ikawa si siri tena. Hilo lilimponza Wenliang mbele ya hukumu za wanasiasa.
Mamlaka za China zilimfungulia mashitaka Wenliang kwa kutoa habari za uongo mitandaoni. Kisha, Wenliang akafutiwa leseni ya udaktari.
Kisha, taarifa za Wenliang zilikifikia Kituo cha Kimataifa cha Udhibiti wa Magonjwa na Kinga (CDC), kisha CDC kwa kushirikiana na WHO, walibaini sifa ya virusi husika na kuviita SARS Coronavirus 2.
Wenliang alisema wagonjwa waliofika au kufikishwa Hospitali Kuu ya Wuhan, walikuwa na alama na dalili kama za SARS, ugonjwa ambao huenezwa na virusi SARS Corona.
WHO walitangaza kuwa ugonjwa uliolipuka Wuhan, China, Desemba mwaka jana na unaoitikisa dunia hivi sasa unaitwa Covid-19 na unasababishwa na maambukizi ya virusi vya SARS Corona 2.
Jiulize; Wenliang alikuwa muongo?
Wuhan ilipozidiwa na wingi wa wagonjwa wa Covid-19, Wenliang alirejeshwa hospitali.
Kisha, Wenliang aliambukizwa Corona katika harakati za kuokoa maisha ya wagonjwa wa Covid-19. Kisha, Wenliang alifariki dunia akiacha mke na mtoto mmoja.
Karne ya 17, Galileo Galileo alikufa dhalili kwa kutengwa, sababu alisema dunia hulizunguka jua. Alizichukiza mamlaka zilizoamini jua ndio huizunguka dunia. Leo, sayansi rasmi inakubali ugunduzi wa Galilei.
Yalimkuta Dk Mwele Malecela aliposema Tanzania kuna vimelea vya Zika. Yamemkuta Dk Nyambura Moremi kwa kuruhusu majibu 'mengi' chanya kuhusu Covid-19.
Ndimi Luqman MALOTO
Tags