Wizara Yazungumzia Watoto Wadogo Waliofunga ndoa


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt Avemaria Semakafu amesema kuwa kwa yeyote aliyehusika ama kuhamasisha vitendo vya ubakaji na ngono kwa watoto wadogo, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 na kwamba lazima sheria itafuata mkondo wake.

Dkt Avemaria ameyabainisha hayo leo Mei 14, 2020, wakati akizungumza na kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa, kuanzia saa 12 Alfajiri hadi saa 4 Asubuhi.

"Mtu yeyote anayetembea na mwanafunzi wa Sekondari ama Msingi ni kitendo cha kubaka, kwahiyo kama kuna hilo tukio limetokea, mpaka linaripotiwa ina maana vyombo vya ulinzi na usalama vimeona, kwahiyo sheria zipo na nadhani ile miaka 15 na 30 inawahusu wahusika wote, hivyo siyo suala la Wizara ya Elimu ni suala ambalo lipo kisheria na misingi ambayo imepitishwa na Bunge" amesema Dkt Avemaria.

Aidha Dkt Avemaria akizungumzia suala la uwepo wa sheria ya kupima mimba watoto watakaporejea mashuleni amesema, "Hakuna sera wala waraka unaotuagiza kupima mimba wanafunzi watakaporejea shuleni, kama Wizara tunachoangalia kwa sasa ni kuandaa mazingira salama ya wanafunzi watakaporejea".

Hivi karibuni liliripotiwa tukio la aina yake, lilionesha watoto wa Darasa la Pili na la Nne wakiwa wamefunga ndoa huko mkoani Geita.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad