Afrika Kusini imesema itaruhusu kufunguliwa tena kwa mikahawa na kumbi za starehe kuanzia Jumatatu inayokuja katika hatua ya hivi karibuni kabisa ya kulegeza vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona licha ya kuongezeka visa vya maambukizi nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na waziri wa Utalii Mmamoloko Ngubane imesema uamuzi huo umefikiwa ili kunusuru sekta ya utalii na biashara baada ya takwimu mpya kuonesha kiasi nafasi 600, 000 za ajira zinaweza kupotea iwapo vizuizi vilivyopo vitaendeela hadi mwezi Septemba.
Ngubane amesema kumbi zote za starehe zitaruhusiwa kufanya kazi kwa asilimia 50 ya uwezo wake huku mikahawa na vituo vya kuuza chakula itaruhusiwa kupokea wateja lakini uuzaji wa pombe bado umepigwa marufuku.
Hadi sasa Afrika Kusini imerikodi zaidi ya visa 118,000 vya maambukizi ya virusi vya corona pamoja na vifo 2,200 huku idadi ya maambukizi mapya ilipanda ghafla siku ya Alhamisi na kufikia visa 6500 kwa siku kutoka visa 1000 mwezi Aprili.