Wakati Shwaibu Jumanne akitafakari jinsi ya kuanza tena maisha uraiani, mambo mawili bado yanamtesa baada ya kukaa mahabusu kwa miaka mitano.
Jumanne, maarufu kwa jina la Mredii, ndiye pekee aliyeepuka hukumu ya kifo wakati Mahakama Kuu ilipotoa hukumu dhidi ya watu sita walioshtakiwa kwa kosa la kumuua mfanyabiashara maarufu wa Mirerani mkoani Manyara, Erasto Msuya.
Washtakiwa wenzake watano wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa, lakini Mredii amerudi uraiani akitafakari maisha mapya baada ya kusimama kazi yake ya uchimbaji madini kwa miaka mitano.
Hata hivyo, tafakuri hiyo inakabiliwa na kumbukumbu mbaya ya tukio lake; kuanzia alipokamatwa hadi maisha ya mahabusu.
“Moja ya mambo ambayo sitakaa niyasahau ni maumivu niliyoyapata wakati nilipokamatwa,” anasema Mrediii katika mahojiano maalumu na Mwananchi baada ya kuachiwa huru.
“Kipigo nilichokipata mikononi mwa polisi kimemsababishia kilema na maumivu.”
Pamoja na kwamba hakusema bayana katika mazungumzo na Mwananchi, Mredii aliiambia mahakama wakati wa utetezi kuwa aliteswa na polisi hadi kupewa ulemavu, ikiwamo kuhasiwa.
Kutokana na kuhasiwa, Mredii alidai aliamua kumpa talaka mmoja ya wake zake, aliyemtaja kuwa ni Zuhura Hassan kwa vile alikuwa hana uwezo tena kama mwanamume. Amebakiwa na mkewe anayeitwa Adile Juma.
Akiongozwa na wakili wake Majura Magafu kutoa utetezi wake, Mredii alidai mbali na kuhasiwa, polisi walimvunja mara mbili mguu wa kushoto na mara moja mguu wa kulia.
Alisema wakati fulani walimfunga kamba na kumning’iniza kama mbuzi aliyebanikwa.
“Kwa hayo mateso niliyopata hapo kituoni nimekuwa mlemavu. Niliwekwa staili ya mbuzi anayechomwa nikiwa sina nguo,” alidai mahakamani.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mredii alisema hakupata matibabu mazuri kutokana na kipigo hicho na kwamba kwa vile sasa yuko huru, moja ya vipaumbele vyake ni kupata matibabu sahihi ya afya yake.
Anasema jambo jingine ambalo hatalisahau ni kulazimishwa kulala saa 9:00 alasiri na kufungiwa vyumbani hata kama huna usingizi. “Wakati mwingine watu wako nje kwenye shughuli zao, lakini sisi tunalazimishwa kulala,” alisema Mredii.
“Hili jambo haliwezi kutoka kwenye akili yangu kwa haraka na litanisumbua kwa muda mrefu sana.
“Kuanzia saa 9:00 (alasiri) mtu unafungiwa ndani, unaambiwa ulale. Kwa kweli yale yalikuwa mateso makubwa kwangu. Halafu chumba kimoja tunalala watu 18 hadi 27. Kwa kweli sitakaa niyasahau maisha haya.”
Hali hiyo ndiyo inamfanya ashauri vijana na watu wengine kutojihusisha na mambo ambayo yanaweza kusababisha wapelekwee gerezani.
“Waepuke kufanya jambo lolote litakalowafanya wapelekwe gerezani kwa kuwa kule ni mahali pa kudhalilisha sana,” anasema.
“Mtu unapokuwa gerezani unakuchukuliwa kama mhalifu na unapokuwa kwenye lile karandinga watu wanaona wewe ni mhalifu na wengine wanakuita mwizi bila kujua ni kosa gani limekupeleka gerezani.
“Lipo suala la matitabu. Mtu anapewa matibabu ya kawaida bila kujali tatizo linalomkabili na ikitokea wakaamua kukupeleka Hospitali za Rufaa nje ya magereza ni kwamba mtu utakuwa umezidiwa.
“Mimi mwenyewe nimetoa matatizo yangu ikiwemo tatizo la vidonda vya tumbo, lakini sijawahi kupimwa licha ya kuomba sana nipelekwe kwenye vipimo ili kujua vidonda vimefikia hatua gani.
“Nimekuwa nikitumia dawa bila kujua (kama) ndizo zinatibu. Sasa natakiwa kwenda kwenye vipimo kwa kuwa kipindi cha miaka mitano nimekaa gerezani (vidonda vya tumbo vimekuwa sugu hasa (kwa kuwa) kule mlo ni mmoja.”
Hukumu ya Mredii na wenzake; Sharifu Mohamed, aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza, Musa Mangu (wa tatu), Karim Kuhundwa (wa tano), Sadik Mohamed (wa sita) na Ally Mussa (wa saba), ilitolewa Julai 23 na Jaji Salma Maghimbi.
Walishtakiwa kwa mauaji ya Msuya, maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, aliyeuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Lakini wakati Jaji Maghimbi aliwapa adhabu ya kifo washtakiwa watano, alimuachia huru Mredii baada ya kutoridhika na hoja za kutaka atiwe hatiani.
Jaji Maghimbi alisema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka haukuweza kuthibitisha shitaka dhidi ya Mredii, hivyo kuamua kumuachia huru.
‘Sikuhusika kupanga wala kushiriki mauaji ya Erasto Msuya na naomba jamii inipokee” alisema Mredii katika mahojiano na Mwananchi.
Anasema uhusiano wake na baadhi ya watu umekuwa ukimtia matatizoni na vyombo vya dola.
“Mwaka 2000 niliwahi kutuhumiwa kwa kosa la mauaji porini Mirerani lakini baada ya upelelezi, nilionekana sikuhusika na kuachiliwa baada ya kukaa mahabusu miezi sita,” alisema Mredii.
“Na hii naona inaweza kusababishwa na hisia kwa kuwa hata tukio linalonikabili naona linaweza kuwa watu wanaangalia ukaribu wangu na watu kwa kuwa Mjeshi ni shemeji yangu.
“Sharifu ni mfanyabiashara ambaye nimekuwa nikimpelekea mawe na hii inaweza kuwa ndiyo iliyosababisha nikahusishwa na matatizo hayo. Lakini namshukuru Mungu na jaji.
“Hakika nilifurahi sana sana kuachiwa na naamini jaji alitumia waledi wake wa kazi kwa kuona kuwa mimi sihusiki na tukio lile, na ukweli ni kwamba mimi sihusiki.” Anasema sasa ana amani kwa kuwa yuko huru.
“Unapokuwa huru, hata kama huna chochote unakuwa na amani. Sitamani kurudi gerezani kwa sababu maisha kule ni magumu sana,” anasema Mredii mwenye watato wanne.
Chanzo: Mwananchi