Amnesty International yakosoa uamuzi wa kuondolewa jina la Saudia katika orodha ya wauaji wa watoto



Shirika la Msamaha Dunia, Amnesty International, limekemea na kukosoa uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kufuta jina la Saudi Arabia na washirika wake karika vita vya Yemen kwenye orodha nyeusi ya nchi zinazoua watoto na kuvunja haki zao.

Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliondoa jina la muungano wa vita huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wauaji wa watoto huku akijua kwamba athari mbaya na haribifu za vita vya Yemen zitaendelea kuvitesa vizazi vijavyo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza kuwa muungano wa vita vya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia umeondolewa katika orodha nyeusi ya taasisi hiyo ya wauaji na wavunjaji wakubwa wa haki zao.

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamemjia juu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kukosoa vikali uamuzi huo.

Human Rights Watch imemkosoa vikali Guterres ikisisitiza kuwa, amepuuza ushahidi wa Umoja wa Mataifa wenyewe, unaoonyesha kuendelea kukanyagwa haki za watoto wa Yemen.

Naye afisa wa shirika la Save the Children, Inger Ashing ameeleza kusikitishwa kwake na 'uamuzi huo wa kutisha' wa Umoja wa Mataifa akisisitiza kuwa umechukuliwa kutokana na mashinikizo.



Kadhalika shirika la kutetea haki za watoto katika migogoro ya kivita (Watchlist on Children and Armed Conflict) limesema kwa kutoubebesha dhima muungano huo vamizi wa Saudia na Imarati, Katibu Mkuu wa UN amewaweka watoto wa Yemen katika hatari zaidi ya kuendelea kushambuliwa.

Mwaka 2017 Umoja wa Mataifa uliiweka Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wauaji na wakiukaji wakubwa wa haki za watoto kutokana na mauaji ya maelfu ya watoto wa Yemen na kuharibiwa shule na mahospitali ya nchi hiyo katika mashambulizi ya Saudia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad