AZIMIO la Bunge la kumpongeza Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa mafanikio katika Bunge la 11 limewagawa wabunge wa upinzani wa vyama vya Chadema na CUF ambapo baadhi wamempongeza wengine wakihoji hatua hiyo.
Wabunge hao walitofautiana jana bungeni wakati wakichangia azimio hilo la Bunge ikiwamo kumpongeza kwa kuitaka Serikali kutobadili uamuzi wa Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi pamoja na matumizi ya vishkwambi ‘tablet’ na kulifanya Bunge kuwa la kisasa katika matumizi ta teknolojia.
Akichangoa azimio hilo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema kuwa hakuna haja ya kumpongeza Spika Ndugai kwani hakuna alichofanya na matumizi ya ‘tablet’ ni jambo la kawaida.
“Tunakuja kupongeza wabunge kutumia kompyuta yaani mabunge mengine wanajadili mataifa yao kufanya utafiti katika Mars kama wanataweza kuuza viwanja leo tunapongeza Bunge kwa Spika kutuletea tablet ni kama umeoa miaka 10 halafu unampelekea mkwe kanga halafu unataka wakwe waje wakupongeze.
“Kuna tofauti kati ya kiburi na ujasiri wajibu wa Bunge ni kuishauri Serikali, tukitaka kupongeza tujiulize Spika amesaidia nini kazi ya Bunge ni uhuru wa Bunge na hili halijawahi kuonekana hadharani uko wapi uhuru wa Bunge leo?.” alihoji Lema.
Lema alisema kwamba azimio la kumpongeza Ndugai lilitakiwa kuletwa katika Bunge lijalo lakini si sasa.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Sonia Magogo (CUF), alimpongeza Spika Ndugai kwa utendaji kazi wake uliotukuka ikiwemo kusimamia nidhamu katika vyama vya siasa.
“Alikuwa na nidhamu katika vyama vya siasa na wale wabunge walioondoka hatupo nao na kama wangeendelea kukumbatiwa tungepata athari kubwa.
“Natambua imani yangu kwamba binadamu hawezi kuwa mkamilifu kwa asilimia 100 natambua kwmba Job Ndugai ni binadamu na kuna sehemu alikuwa anateleza kama binadamu. Mimi namwelezea kama ni Spika ambaye ni msikivu ana ubinadamu amekuwa ni jasiri na mtu ambaye hayumbishwi
“Ameonesha ujasiri mkubwa katika janga la Corona na kama Bunge lingefungwa lingeleta taharuki amesimamia marekebisho ya sheria,” alisema Magogo
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema hakuna haja ya kumpongeza Spika Ndugai, kwani katika kipindi cha uongozi wake ndicho ambacho Bunge limekosa demokrasia.
“Kwa maoni yangu wakati wa Bunge la 10 ndiyo demokrasia ilikuwa inapaa ila hili Bunge limeshusha kwa kiwango kikubwa sana demokrasia Bunge hili linanyima uhuru wa mawazo,” alisema
Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Tabora Mjini Emmanuel Mwakasaka (CCM), alisimama na kumpata taarifa Msigwa kwa kudai kwamba kama anasema wamenyimwa uhuru wa kuzungumza mbona muda huo amepewa nafasi ya kuzungumza na anazungumza?
“Hawapewi nafasi ya kusema sijui ni ipi labda aseme anafanya nini hapo?.” alihoji Mwakasaka.
Msigwa hakumjibu Mwakasaka na badala yake akaendelea kuchangia kwa kudai kwamba Bunge hili ndilo ambalo limezuia Speech za wapinzani kusomwa.
Wakati akiendelea kuchangia Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel alisimama na kumpa taarifa Msigwa kwamba yeye Msigwa ndiye aliyelipotosha Bunge kwa kusema Kinana ni jangili.
Akimjibu Msigwa alisema : “Watu wanaaomba msamaha ni wenye nguvu na niliyemuomba msamaha amenielewa na amesema mimi ni muungwana,”.
“Hatujaja hapa kupigiana makofi kamaNdugai anafanya vizuri kizazi kijacho kitakuja kusema hili ni Bunge limewatisha watu mnaposema tusizungumze tukazungumzie wapi?.” alisema
Baada ya kumaliza kuchangia Msigwa, Naibu Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson alisema: “ Tusome vizuri vishwambi vimetajwa kama mfano ni hapa mabadiliko ni kwenda kwenye Bunge mtandao,”.
Mbunge wa Viti Maalum,Amina Molel (CCM) alisema ni lazima Spika Ndugai,. apongezwe kwani ameweza kulifanya Bunge hilo kuwa la kisasa.
Mbunge wa Viti Maalum Felister Bura (CCM) alimpongeza Spika kwa kuwa jasiri na mara zote kusimamia haki katika kila jambo.
“Tume alizoziunda Spika ndio matunda yake haya unawezaje kutaja mafanikio bila ya kutaja mafanikio ya Spika kwa upande wa Dodoma Ndugai anapita bila kupingwa unaposema tusimpongeze Spika mimi hata sikuelewi,” alisema.