Bei ya ufuta yaongezeka kwa mwendo wa pole Lindi Mwambao



Na Ahmad Mmow, Lindi. 

Bei ya ufuta katika chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao imeongezeka baada ya leo katika mnada wa zao hilo uliofanyika katika mtaa wa Tulieni, manispa ya Lindi kununuliwa kwa bei ya juu ya shilingi 2115 na bei ya chini ni shilingi 2046. 

Bei ambazo nitofauti na mnada wa kwanza katika msimu huu wa 2020 uliofanyika tarehe 6.6.2020 katika mtaa wa Ng'apa, manispaa ya Lindi. ¥ Katika mnada huo barua 14 za kampuni ziliomba kununua zilisomwa. Huku ikishuhudiwa kampuni za HS Impex, Export Trading Ltd, Tapal, UR OM, Afrisian, SM Holdings na Hy seas zikifanikiwa kununua ufuta wote wenye uzito wa kilo 2,945,364 uliopo katika maghala ya Bucco, Nangurukuru na Mtama. 

Aidha ghala la Nangurukuru lilipo wilayani Kilwa limeongoza kwakuwa na ufuta mwingi. Kwani linaufuta wenye uzito wa kilo 1,359,163. Wakati ghala la Bucco likifuatia kwakuwa na ufuta wenye uzito wa kilo 967,428. 

Huku ghala la Mtama likiwa na kilo 618,773. 

Akizungumza kwenye mnada huo baada ya wakulima kukubali kuuza kwa bei hizo, makamo mwenyekiti wa Lindi Mwambao, Rashid Masoud aliwatahadharisha wakulima wasichanganye uchafu kwenye ufuta ili kuongeza uzito. Akiweka wazi kwamba licha ya kitendo hicho kusababisha kushusha bei za zao hilo sokoni, lakini pia ni kosa. 

Masoud alisema amesikia tetesi kwamba kuna tani 15 za makinikia ya ufuta yaliyotoka viwandani zimeletwa na kuingizwa katika mkoa wa Lindi ambazo wanauziwa wakulima ili wachanganye kwenye ufuta wao waongeze uzito. 

'' Watu hao wasio tutakia mema wanauza kwa wakulima makinikia hayo kwa bei ndogo ili kuwauzieni wakulima. Msikubali kununua mtapata matatizo,'' alionya Masoud. 

Katika kukabiliana na hujuma hiyo, makamo mwenyekiti huyo aliagiza vyama vyote vya msingi vya ushirika vinavyounda chama kikuu hicho vinunue matarubai yatayotumika kumiminia ufuta wa wakulima ili kukagua kabla ya kupima uzito. 

Mbali ya hayo Masoud licha ya kuwapongeza wanunuzi walionunua ufuta katika mnada wa kwanza kwa kulipa fedha za wakulima aliwataka waondoe mizigo yao kwenye maghala ndani ya muda ulipangwa kisheria na waendelee kulipa fedha za wakulima kwa wakati. 

Katika mnada wa kwanza bei ya juu ya zao hilo ilikuwa shilingi 2,112 na bei ya chini shilingi 2,053 kwa kila kilo moja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad