Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said.
MKURUGENZI Uwekezaji wa GSM na Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said, ameibuka na kufunguka mengi mazito juu ya mkataba na hatma ya kiungo wao mshambuliaji, Mghana, Bernard Morrison.
Hiyo ikiwa siku moja imepita tangu Mghana huyo aweke wazi juu ya mkataba wake ambao unamalizika mwezi ujao huku akikanusha kuongeza mwingine wa miaka miwili kusalia klabuni hapo.
Mghana huyo alijiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akisaini mkataba wa miezi sita kabla ya uongozi wa timu hiyo kutangaza wamemuongezea mwaka mmoja na nusu utakaomalizika Julai 2022.
Akizungumza na Spoti Xtra, Said alisema kuwa hakuna kitu kingine kinachoendelea kwa Morrison zaidi ya tamaa, kwani yeye mwenyewe anafahamu ana mkataba wa miaka miwili na Yanga aliousaini hivi karibuni baada ya kuona ule wa awali kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
Said alisema kuwa Mghana huyo alianza visa muda mrefu ndani ya timu hiyo baada ya kumgomea kuvunja mkataba wa kuendelea kuichezea Yanga siku chache tangu apate ofa nzuri kutoka timu mbalimbali zikiwemo za Uarabuni na Afrika Kusini.
“Niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kuwa, Morrison alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga ambao uliwasilishwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) pamoja na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa).
“Baada ya kusaini mkataba huo, baadaye alitufuata viongozi na kuomba kuuvunja kwa sababu amepata ofa nzuri zaidi kwenye klabu nyingine.
“Kama klabu tunasimamia misingi na kama kuna timu inamuhitaji Morrison waje tukae meza moja tuzungumze, sisi tupo tayari kumuuza, hapa hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu.
“Morrison alianza visa mchezo wa kirafi ki na KMC ambao alitakiwa awepo kambini lakini hakutokea, tumesafiri kwenda Shinyanga akagoma, akaambiwa ataenda kwa ndege na kocha, alimhakikishia, lakini bado hakusafiri na kuchukua uamuzi wa kuzima simu yake, huu ni utovu wa nidhamu.
“Hatutalifumbia macho hili la Morrison, tayari tumeiandikia barua TFF juu ya hilo na lazima haki itendeke, hivyo tutakutana kwenye haki,” alisema Said.
Wakati sakata hilo likiendelea, Yanga kupitia kwa kaimu katibu wake, Wakili Simon Patrick, jana ilitangaza kukata sehemu ya mshahara wa kiungo huyo kiasi cha Sh 1,500,000 kwa mujibu wa kanuni na taratibu za klabu hiyo kutokana na kile kilichoelezwa ni kukiuka taratibu hizo akiwa na nia ovu.