CHADEMA yajitosa kinyang'anyiro cha Urais Zanzibar, Watia Nia Wapewa Siku 10
0
June 07, 2020
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa upande wa Zanzibar kimetangaza kushiriki kugombea nafasi ya Urais wa Zanziabar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu.
Akitangaza uamuzi huo mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa upande wa Zanzibar, -Salum Mwalimu amewataka wanachama wa chama hicho wenye sifa na maadili kujitokeza na kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
Amesema Mwanachama yeyote mwenye nia ya kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar kuanzia leo anaweza kupeleka barua ya maombi katika mamlaka zinazohusika ndani ya CHADEMA na kwamba zeozi hilo la siku kumi litafika tamati Juni 16 mwaka huu.
Aidha, Mwalimu amewataka wanachama wa chama hicho walioko nje ya nchi kwa sasa, kuwasiliana na ofisi yake ili wapewe utaratibu wa kuwasilisha kusudio lao la kugombea Urais Zanzibar kupitia Chadema.
“Kwa wale ambao taarifa hizi za kutangaza nia zitawakuta nje ya Zanzibar, wanaruhusiwa kufanya mawasiliano na ofisi Naibu Katibu Mkuu Zanzibar ili tuweze kuwawekea utaratibu upi wa kuweza kuwasilisha kusudio lao hilo la kugombea Urais Zanzibar kupitia Chadema,” amesema Mwalimu.
Amesema, pamoja na tangazo hilo, chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, “kipo tayari kuendeleza ushirikiano na vyama na kulinda nia na shabaha ya ushirikiano huo bila kuathiri malengo ya vyama vyetu kwa masilahi ya kila Mzanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.”
Tags