Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi, Bw.Abdulrahaman Kinana amemuomba radhi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa matukio mbalimbali aliyoyafanya baada ya kuondoka katika uongozi wake.
Pamoja na hayo Kinana amewaomba radhi pia Watanzania na Wanachama wa CCM kwa vitendo alivyovifanya.
Kinana akiwa na baadhi ya viongozi wakongwe wa chama hicho walipewa adhabu baada ya mazungumzo yao ya simu kunaswa wakimteta Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii hali iliyosababisha uongozi wa CCM kuwaita na kuwahoji viongozi hao.
Awali akizungumzia adhabu aliyopewa na chama Kinana amekiri kutokea kwa jambo hilo na kudai kuwa kama binadamu alighafilika na kudai kuwa akiwa ni mkongwe katika chama hicho adhabu ni utaratibu uliopo katika chama chochote kwa kiongozi au mwanachama anapokosea.
Wakati huo huo Komrade Kinana ametembea ofisi za CCM mkoa wa Arusha na kuzungumza na mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha Zelothe stephen zelothe.
Tangu sakata hilo litokee Katibu mkuu huyo mstaafu wa CCM hakuwahi kusikika katika vyombo vya habari wala mitandao ya kijamii kuzungumzia sakata hilo.