Maafisa wa usalama nchini Iraq jana wamevamia makao makuu ya kundi la wanamgambo wenye nguvu wanaungwa mkono na Iran kusini ya mji mkuu Baghdad na kuwakamata makamanda watatu wa kundi hilo pamoja na maroketi kadhaa.
Maafisa wa serikali ya Iraq wamesema uvamizi huo umelilenga kundi la Kataib Hezbollah lenye mafungamano na Iran ambalo maafisa wa Marekani wamelituhumu kwa kurusha maroketi kwenye kambi zake za kijeshi na vituo vyake vingine nchini Iraq.
Huo ni uvamizi wa aina yake kuwahi kufanywa na maafisa wa usalama wa Iraq dhidi ya kundi hilo lenye nguvu ambalo matawi yake ya wapiganaji wenye silaha yameimarisha udhibiti wa kijeshi kisiasa na kiuchumi nchini Iraq.
Operesheni hiyo iliyofanywa usiku wa maneno ni ishara ya kwanza kuwa waziri mkuu mpya wa Iraq Mustafa al-Kadhimi anatimiza ahadi yake aliyoitoa ya kuchukua hatua kali dhidi ya makundi yenye silaha yanayolenga miundombinu ya Marekani nchini humo.