Katika kuendelea mvutano kati ya Cairo na Addis Ababa kuhusu bwawa la An Nahdhah, naibu mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Ethiopia amesisitiza kuwa nchi hiyo itatetea kwa nguvu zake maslahi yake katika bwawa hilo.
Luteni Jenerali Birhanu Jula, Naibu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Ethiopiia amesema katika radiamali yake kufuatia kuongezeka hali ya mvutano kati ya nchi hiyo na Misri kuhusu bwawa la An Nahdhah kuwa Addis Ababa haitafanya mazungumzo kuhusu mamlaka yake katika mpango ambao umezusha hitilafu kubwa kuhusu suala hilo baina yake na Misri.
Jula ameongeza kuwa Misri na walimwengu wanafahamu kuwa taifa la Ethiopia ni jasiri ambalo haliogopi mauti na linajua vyema jinsi ya kuendesha vita iwapo litalazimika.
Naibu Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Ethiopia aidha ameituhumu Misri kuwa inatumia silaha kuzitishia nchi nyingine ili zisitumie maji ya pamoja na kusisitiza kuwa nchi zinapasa kushirikiana kiuadilifu ili kusonga mbele.
Bwawa la An Nahdhah linajengwa katika Mto Blue Nile nchini Ethiopia na katika umbali wa kilomita 40 katika mpaka wa Sudan. Ethiopia ilianza kujenga bwawa hilo mwezi Apili mwaka 2011 hata hivyo hitilafu kali kati yake na Misri na Sudan zimechelewesha ujenzi wake.
Cairo inaamini kuwa ujenzi wa bwawa la An Nahdhah unaathiri vibaya mgawo wa maji wa Misri wa kila mwaka kutoka mto Blue Nile hata hivyo Ethiopia kwa upande wake inasema kuwa ujenzi wa bwawa hilo hauzisababishii madhara Misri au Sudan.