Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imefungua majalada 23 ya kesi za rushwa ya ngono, kumi kati ya hizo zikisikilizwa na tano kushinda katika mikoa mbalimbali.
TAKUKURU pia, imewataka wakuu wa vyuo kusimamia suala la rushwa ya ngono vyuoni ili kusaidia kupunguza ukandamizaji unaofanywa hususani kwa watoto wa kike.
Hayo yamesemwa Juni 18,2020 jijini Dodoma na mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini,Brigedia Jenerali John Mbungo wakati akifungua warsha ya utafiti wa rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu ,uchunguzi wa kifani wa vyuo vikuu vya Dar Es Salaam na Dodoma iliyoandaliwa na Taasisi ya kiraia ya Mfuko wa Wanawake Tanzania[Women Fund Tanzania] .
Brigedia Jenerali Mbungo amesema kufuatia kuwepo kwa malalamiko ya rushwa ya ngono Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini [TAKUKURU]ilitoa tamko la kushughulikia taarifa za malalamiko ya rushwa ya ngono ambapo kuanzia mwaka 2013 hadi machi 2020 jumla ya majalada 23 yalifunguliwa kwa mikoa 14 ya Tanzania.
Brigedia Mbungo amesema mkoa wa mwanza majalada 4 Yalifunguliwa,majalada 3 kwa kila mkoa katika mikoa mitatu ya Kagera,Mtwara na Mara na jalada 1 kwa kila mkoa katika mikoa 10 ya Arusha,Dodoma ,Geita,Iringa ,Katavi,Kinondoni,Manyara,Rukwa ,Singida na Temeke.
Aidha.Brigedia Mbungo amesema jumla ya kesi 10 zilizofunguliwa Mahakamani,kesi tano zishinda na kati ya hizo nne zilihusu taasisi za Elimu,kesi 3 zilishinda kesi moja iliondolewa mahakamani na kesi moja inaendelea Mahakamani ambapo majalada 10 yanaendelea na uchunguzi ambapo katika jitihada za kudhibiti rushwa ya ngono TAKUKURU kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania wamezindua kampeni ya Vunja Ukimya kataa rushwa ya ngono .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya mfuko wanawake (WFP) Prof.Ruth Meena amesema kuwa Pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Serikali kuwalinda watoto wa kike bado wanakabiliwa na kupewa vitisho wanapotaka kujinasua katika rushwa ya ngono.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Door of Hope Tanzania Clemente Mwombeki amesema kuwa Jamii bado haina uelewa juu ya madhara ya rushwa ya ngono hali inayokwamisha juhudi za wanaharakati Katika kufuatilia ukatili huo.
Mwanasheria wa TAKUKURU kupitia Idara ya Uzuiaji Rushwa Denis Lekayo amesema kumekuwepo na baadhi ya wanawake kutengeneza mazingira ya kushawishi rushwa ya ngono .
Mwisho.