Kiba Ampindua Mondi, Harmo Kibabe!




DAR: Mara paap! Mwenye muziki wake huyu hapa, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ameibuka na kuwapindua vibaya wenzake; Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’ ambao walikuwa wamejihakikishia ufalme wao kwenye gemu, Gazeti la IJUMAA limekukusanyia habari.

 

NI PALE KIJIJINI YOUTUBE

Kabla King Kiba hajaibuka na kuwavuruga watu, Diamond au Mondi na Harmonize (Harmo), wao ndio walikuwa wamelikamata soko la muziki kwa kuwa kwenye nafasi za juu kwenye Mtandao au ‘Kijiji’ cha YouTube.

 

Kwa nyakati tofauti, Mondi aliishikilia namba moja kwenye ‘trending’ huku Harmo akimsogelea mara kwa mara kuashiria anataka kumuondoa.

 

NYIMBO ZAO

Mondi na kijiji chake cha Wasafi, alikuwa akisumbua na Wimbo wa Quarantine ambao amefanya na vijana wake wote; Rayvanny, Mbosso, Lava Lava, Queen Darleen na Zuchu.

 

Wimbo huo ambao aliuachia Mei 22, mwaka huu, ulijichimbia kwenye nafasi ya kwanza kwa wiki kadhaa huku Harmo akija kwa kasi na wimbo wake wa Falling in Love, lakini akaishia namba mbili.

 

Harmo aliuachia wimbo huo Mei 28, mwaka huu ambao ulikwenda kwenye nafasi ya pili na kuwa gumzo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

 

GUMZO LA NINI?

Gumzo kubwa lililokuwa likijadiliwa ni kama anaweza kumtoa kwenye reli bosi wake wa zamani, Mondi lakini hata hivyo, hakuweza kufanikiwa, anahitaji pumzi ya ziada.

 

KING KIBA AIBUKA SASA

Juni 8, mwaka huu, Kiba aliibuka ghafla na wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la So Hot na siku iliyofuata tu (Juni 9) ngoma hiyo iliwashusha wasanii wote kwenye chati akiwemo Mondi mwenyewe na Harmo waliokuwa wamejihakikishia nafasi za juu.

 

NI REKODI YA KIBABE

Hiyo ikawa ni rekodi ya kibabe kwa King Kiba, kwani ameweza kuwaondoa wawili hao na wengineo ndani ya saa kadhaa tu tangu aipakie ngoma hiyo kwenye akaunti yake ya YouTube akitumia jina la Kings Music.

 

MAONI KAMA YOTE

Maoni kama yote yalimiminika kwenye Mtandao wa YouTube ambapo wafuasi wa staa huyo walimpongeza kwa kuwaondoa Mondi na Harmo.

 

“Hii ni mara ya tano sasa naiangalia hii ngoma tangu itoke, hebu gonga ‘like’ kama umeikubali kama mimi.”

“Kumbe anayeweza kumtoa Mondi kwenye trending ni Kiba pekee coz Harmo alishindwa.”

 

“Jamani mbona tunazembea ngoma ipo no 1 on trending halafu one million bado, hebu tuliamshe dude one million ifike now So Hot.”

Hayo yalikuwa ni baadhi ya maoni ambayo yalitolewa na watu mbalimbali kumpongeza Kiba.

 

MTAALAM AFUNGUKA

Akizungumzia kitendo cha Kiba kuibuka na kuwapindua ghafla wenzake waliomtangulia kuachia ngoma, mtaalam wa masuala ya IT, Edwin Lindege, alisema Kiba amefanikiwa kutokana na jinsi watu walivyokuwa wakiigombea kuitazama ngoma hiyo, hivyo kuifanya iwe trending.

 

“Baada tu ya kuiachia, inaonekana aliwapa watu wengi link na wengine kuiona kwenye ukurasa wake wa Instagram, hivyo kufanya awe na idadi kubwa ya watu wanaoiangalia kwa wakati mmoja.

 

“Wanachoangalia YouTube hadi wimbo au kazi yako iwe trending, ni kile kitendo cha watu kuigombea kwa wakati husika ndiyo maana unaona inakuwa trending, lakini ukitazama views (idadi ya watazamaji) husika wanakuwa bado wapo chini.

 

“Hivyo huyo King Kiba akiendelea kufanya vurugu za kushea link, anaweza akafikisha idadi kubwa sana ya watazamaji (views) ndani ya muda mfupi,” alisema Lindege.

 

KIBA ANASEMAJE?

Akizungumza kuhusu jambo hilo alipotembelea Global Publishers juzi Jumatano, Kiba alisema anamshukuru Mungu na mashabiki wake kwa kuifanya ngoma yake iongoze.

“Mimi nasema asante kwa Mungu, lakini pia nawashukuru sana mashabiki maana wao ndiyo wameamua kuniweka hapo,” alisema King Kiba.

 

KUHUSU MONDI…

Alipoulizwa kuhusu kuwashusha Mondi na Harmo, alisema yeye asingependa kuwaongelea hao, lakini kubwa zaidi ni kuwashukuru mashabiki kwa kuendelea kumuunga mkono.

 

TAKWIMU ZILIVYO YOUTUBE

Hadi juzi, So Hot ambayo ilikuwa inaongoza kwa kuwa trending YouTube, ilikuwa imetazamwa mara zaidi ya laki 7 huku Falling In Love wa Harmo ukiwa na watazamaji zaidi ya milioni 2, lakini ikiwa namba 8 kwenye trending.

 

Quarantine ya Mondi na vijana wake ulikuwa umetazamwa mara zaidi ya milioni 6,387,575 ikiwa imekamata namba 5 katika trending.

Stori: ERICK EVARIST, Ijumaa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad