KOCHa wa zamani wa Klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa amekosa nafasi ya kwenda kuinoa Klabu ya Township Rollers kutoka Gaborone nchini Botswana kwa sababu hajui kuongea Kiingereza.
Zahera amesema siyo timu hiyo pekee ambayo ilikuwa inahitaji huduma yake bali hata baadhi ya timu kutoka Afrika Kusini zilimpigia simu lakini yeye akagoma kwa sababu hawezi kuzungumza Kiingereza na hapendi kuwa na mkalimali katika kazi zake.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema amepigiwa simu na mawakala kutoka Botswana wakimueleza kwamba klabu hiyo inatafuta kocha na yeye wamemuona atawafaa kwa kuwa hana timu ila yeye
aliwajibu kuwa hawezi kuzungumza Kiingereza vizuri hivyo itakuwa ngumu kwake kuwasiliana na wachezaji pamoja na viongozi.
“Wakala kutoka Botswana alinipigia simu akaniambia kuwa Township Rollers wanahitaji kocha na wameona mimi nawafaa, lakini nikawaambia kuwa mimi siwezi kuongea Kiingereza na sitakuwa huru kufanya kazi nikiwa na mkalimani na siyo hao tu, kuna timu nyingine kutoka Afrika Kusini zilikuwa zinanitaka pia,” alisema Zahera