MWIGIZAJI nguli wa vichekesho Bongo, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, ameibuka na kuonesha pesa na utajiri wake anaomiliki uliotokana na kazi yake hiyo ya kuvunja watu mbavu.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Kingwendu amesema kuwa, sanaa yake imempa mafanikio makubwa, kwani anamiliki vitu vya thamani kutokana na kazi yake hiyo.
“Mimi ninamshukuru sana Mungu, tangu nilipotoka mpaka nilipo sasa, kwani nimepata mafanikio makubwa; nini magari? Nyumba ninazo, nimejenga nyumba kubwa tu maeneo ya Mbagala, namiliki magari matatu; Toyota Crown (Paka Mweusi) ambayo imenigharimu Sh milioni 25, Toyota Prado Old Model, kwa sasa liko Arusha kwa ajili ya kusafirisha watalii, Toyota Noah, bodaboda, saluni mbili na duka.
“Nina mpango wa kufungua kampuni yangu mwenyewe kupitia jina langu la Kingwendu.
“Pia kwa sanaa yangu nimeweza kusomesha watoto. Hayo ndiyo mafaniko ninayojivunia.
“Namshukuru sana Francis Ciza (Majizo) ambaye ni Mkurugenzi wa E-FM, kwani amenisimamia sana katika kazi zangu. Hata wazo la kwenda kutangaza pale kwenye redio yake (E-FM), yeye ndiye alitoa hilo wazo, maana nilienda katika kipindi tu kama mgeni, ndani ya mwezi mmoja, wakawa wananipa majaribio ya kusoma magazeti nikiwa na Steve Nyerere. Majizo na wafanyakazi wake wakaona kipaji changu, nikabaki kuwa kama mtangazaji mpaka sasa,’’ amesema Kingwendu.
Kingwendu amesema kuwa, wasanii wengi wamekuwa wakijisahau sana kwa kufanya starehe na si maendeleo.
“Wasanii wamekuwa wakikimbilia kuanza kununua magari badala ya kujenga kama jinsi nilivyofanya,” amesema Kingwendu.
Kingwendu ni mwigizaji wa vichekesho ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kupitia kazi zake. Amecheza filamu nyingi akiwa na wachekeshaji wakali hapa Bongo.