Kizungumkuti kipya mpaka wa Tanzania na Kenya





MPAKA wa Namanga upande wa Tanzania umeendelea kusitisha shughuli za kibiashara na Kenya, baada ya kuibuka hali ya sintofahamu kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili. 

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kenya kukiuka makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo mbili Mei 22 mwaka huu, ambapo maofisa wa Kenya wanadaiwa kukataa kuwapokea madereva wa magari ya mizigo kutoka Tanzania  ambao wamepimwa na kuonekana hawana corona. 

Kitendo cha upande wa Kenya kuwazuia madereva wa Tanzania wenye vyeti vya uthibitisho kinatajwa kuwa kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa na mawaziri wa uchukuzi kutoka nchi hizo mbili na watendaji wengine wa Serikali. 

Makubaliano ya watendaji hao katika nchi hizo mbili ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Marais Dk. John Magufuli na Uhuru Kenyatta waKenya, kuwataka watendaji hao kukutana na kujadiliana namna ya kutatua mgogoro uliosababisha mikapa hiyo kufungwa. 

Kabla ya agizo hilo la wakuu wa nchi, mbali na Namanga, mipaka mingine iliyokuwa imefungwa ni Olili ulio Kilimanjaro, Horohoro ulio Tanga na Sirari, Mara. 

Akizungumza na MTANZANIA JUMAPILI, Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, amethibitisha kufungwa kwa mpaka wa Namanga kuanzia Juni 3. 

Alisema madereva wa Tanzania wamelalamika kuwa vyeti vyao vimekuwa vikikataliwa wanapoingia nchini Kenya, hali inayosababisha taharuki. 

Alisema baada ya suala hilo kuibuka alijaribu kuwashirikisha viongozi wa wilaya ya Kaijado (Kenya), ambao nao walidai siyo wasemaji katika suala hilo hivyo hawawezi kusema lolote. 

Alisema juhudi za kutatua changamoto hiyo ziliendelea ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliwasiliana na Gavana wa Kaijado ambaye pia hakutoa ufumbuzi wa suala hilo. 

 “Pamoja nakujitahidi kuwasiliana na wizara husika bado ushirikiano ulikuwa hafifu, tulisubiri Juni mosi, mbili hadi tatu hali iliendelea kuwa hivyo. Madereva wakaendelea kulalamika sasa haiwezekani madereva wamepimwa siku mbili zilizopita anarudia kwenda kupima eneo lingine wakati siyo makubaliano,”alisema. 

Alisema kuanzia Mei 31 mwaka huu madereva wa malori kutoka Tanzania, licha ya kuwa na vyeti vya uthibitisho kutoka kwa wataalam wa afya vinavyoonyesha hawana maambukizi, bado Kenya wanawakaa. 

 “Mpaka umefungwa tangu Juni 3 mwaka huu, sisi hatukuwa na shida kuhusu vyeti vyao, wanalazimisha madereva wetu wapime tena wakati siyo haki, tulishakubaliana kila upande upime watu wake nakuwapa vyeti. Sisi tunatekeleza yale Rais alichoagiza kifanyike, tumetekeleza wenzetu tunaona hawajatekeleza,”alisema. 

 Alisema kwasasa hakuna shughuli zinazoendelea na katika mpaka wa Namanga na kuna magari zaidi ya 500 yanayosubiri kuingia Kenya. 

Kwa upande wao baadhi ya madereva hao walisema mambo yanayojitokeza sasa katika maeneo ya mipaka hayaathiri wafanyabiashara pekee, bali ushirikiano wa wanajamii katika nchi hizo mbili. 

Holili 

Hali kama hiyo pia ipo katika mpaka wa Holili mkoani Kilimanjaro, ambapo pia madereva wanadai wakiingia Kenya vyeti vyao vinakataliwa. 

Fransis Mtui ambaye ni mmoja wa dereva alisema  kitendo hicho ni kuidharau Wizara ya Afya ya Tanzania hivyo kuiomba Serikali iweke misimamo ili vipimo vyao  viheshimiwe. 

“Tuumeshapima Arusha na majibu yamerudi lakini tumefika hapa wenzetu upande wa Kenya wamekataa, hawavitambui vipimo vya Tanzania wanataka lazima tupimwe upya, wengine wamekubali kwasababu wanaogopa kupoteza kazi, matajiri wetu wamesema tupimwe tu, “alisema Mtui. 

Azizi Juma alisema amekaa zaidi ya siku tano kutokana na cheti chake kukataliwa hivyo kuzuiwa kupita  nakurudia kupimwa upande Kenya ambapo hadi sasa hajapata majibu. 

“Nilipimwa Arusha wakati nakuja na nilikaa Arusha zaidi ya siku nne kusubiri majibu yakarudi Sina corona na nikapewa cheti ili niweze kusafirisha mizingo lakini nimefika hapa hataki kuitambua, “alisema. 

Ofisa Mfawidi mpaka wa Holili, Mahamood  Makami alisema, Kenya wamekiuka makubaliano waliokubaliana viogozi wa pande zote mbili katika kikao kiliyofanyika Mei 22,2020 Namanga jijini Arusha. 

Alisema makubaliano ni kwamba madereva wakishapimwa Tanzania nakupatiwa cheti cha vipimo vya corona, aruhusiwe kupita katika mpaka. 

“Lakini wenzetu hawataki wanataka wapimwe upya ndipo wapitie hali ambayo ni kinyume na makubaliano ya awali,” alisema. 

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingireza (BBC), madereva wa Kenya wamekiri kuwepo kwa changamoto kwa madereva wa Tanzania wanapoingia upande wa Kenya. 

”Upande wetu wa Kenya hawazingatii kama Tanzania inavyozingatia sisi kwao, wanatukubalia kutumia cheti tunachotoka nacho Kenya lakini Kenya hawakubali vyeti vya madereva wa Tanzania,” alisema Joseph Kariuki. 

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe, alisema madereva wote wa malori lazima wapime virusi vya corona angalau saa 48 kabla ya kuanza safari. 

”Tumegundua kuwa madereva wengi huanza safari kabla ya kupimwa na kupata nyaraka muhimu, wakitegemea kupimwa kwenye eneo la mpaka, hali inayosababisha msongamano usio wa lazima na ucheleweshaji katika maeneo ya mipaka yetu, huku ni kutokuwa na nidhamu jambo ambalo halikubaliki na halitavumilika, ninawataka maofisa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya madereva wanaolikuka utaratibu. 

”Wengine wanafika boda wakiwa na vyeti vyao wanafuata sheria, lakini wanakaa siku mbili kwa kuwa kuna wasio na vyeti wamezuia barabara, hata ukiangalia unaona kuna shida ya watu kutokuwa na nidhamu. 

”Tuna shida pia upande wa Tanzania, hayo ni mambo mengine na tunasema ukija lazima uwe na cheti na ukiwa huna cheti huwezi ingia Kenya, kama ambavyo Mkenya ilivyo kwake hawezi kuingia Uganda au Tanzania kama hana cheti,” BBC ilimnukuu Kagwe. 

Alisema cheti kinachotakiwa lazima kiwe chenye maana kinachotambulika na maabara inayotambulika na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Tatizo ni kuto Elewa?
    Au ni utukutu wa Kuto tii Amri.

    Mabalozi hii ni saizi yenu na Wizara
    Shirikishi.

    Magu na Uhuru yao walishamaliza hawa
    ndugu wawili. Au mnataka Utumbuzi?

    it did not work..?? Sit down Again.!!!

    We need Solutions rather than propagation in Media.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Na kama, Itabidi.
      Basi Kikosi kazi kiundwe pande zote mbili. with legal framework to monitor its implementation andits achivment.

      its a failure which we cannot afford to see. while we are members in current goverment with decision capacity and we fail..????

      Move on with solution in hand.
      Be performer..!!
      Be achiever..!!

      Work for the people . Be an EAC ICON. With unsurpased patriotism

      By Wednesday it should be DONE.

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad