Marekani imepoteza watu 687 kutokana na virusi vya korona leo, ikiwa ni siku ya nane mfululizo kwa idadi ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo ya COVID-19 kuwa chini ya 1,000 kwa siku.
Ujerumani imesajili watu wengine 504 walioambukizwa virusi vya korona hivi leo, na kuifanya idadi ya watu waliokwishapata maradhi ya COVID-19 kufikia 188,534.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Robert Koch, watu wengine 16 wamepoteza maisha ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, vifo ambavyo vinaifanya idadi ya waliokwishapoteza maisha kwa ugonjwa huo kufikia 8,872.
Marekani kwa upande wake, imepoteza watu wengine 687 kutokana na virusi hivyo hivi leo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Hii ni siku ya nane mfululizo kwa idadi ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo ya COVID-19 kuwa chini ya 1,000 kwa siku, licha ya nchi hiyo ikisailia kuwa taifa lililoshambuliwa sana na janga hilo, ambapo hadi sasa limeshapoteza watu 118,381, kati ya milioni 2, 187,876 walioambukizwa.
Baadhi ya majimbo yameshuhudia kurejea upya kwa kasi ya maambukizo, wakati kiini cha mripuko huo kikiondoka kutoka jiji la New York na kuelekea Kusini na Magharibi.
Katika taifa jirani, Mexico, wizara ya afya ya nchi hiyo imesajili watu wengine 5,662 walioambukizwa ugonjwa huo, na vifo vipya 667, idadi ambayo inawafanya waliokwishaambukizwa kufikia 165,455 na waliokwishafariki kuwa 19,747.
Serikali inasema idadi kamili ya waliokwishaambukizwa huenda ikawa ni kubwa zaidi ya iliyochapishwa.