MADARAKA Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ametangaza kuwania nafasi ya ubunge wa Butiama mkoani Mara, kupita Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Madaraka ambaye ni mtoto wa sita kwa kuzaliwa kati ya watoto wanane wa Mwalimu Nyerere, alitangaza nia hiyo jana nyumbani kwao Mwitongo, Butiama saa chache baada ya Rais John Magufuli kuvunja Bunge.
“Sijatumwa na mtu yeyote kuomba nafasi hii ila nimejipima uzoefu na uwezo wangu na kuamua kuwa ni wakati mwafaka sasa wa kutumia uwezo na uzoefu huo kutumikia jamii pana zaidi,” Madaraka aliwambia waandishi wa habari na kuongeza: “Ni kwa sababu sijatumwa na mtu ndio maana leo (juzi) hii mnaniona niko hapa peke yangu kutoa tamko hili, kwa sababu pamoja na kwamba nahitaji uungwaji mkono wa Chama Cha Mapinduzi na wapigakura wa Butiama, hatua ya kwanza ninataka kuifanya mwenyewe kwa kuamini kwamba ninaweza kupokea majukumu nitakayokabidhiwa.”
Aliweka wazi jambo la kwanza lililomsukuma kuwania nafasi hiyo kuwa ni baada ya kuona Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Magufuli amejenga mazingira mazuri yanayomwezesha mwanachama yeyote wa chama hicho kugombea uongozi na kupata haki bila kujali uwezo wake wa kifedha wala ukaribu wake na viongozi wa juu.
“Pili, Magufuli ni kiongozi ambaye tumeona ameweka jitihada kubwa za kutanguliza maslahi ya taifa mbele, kwa hiyo katika mazingira kama hayo na mimi nikijipima na imani zangu nafikiri itakuwa ni heshima kubwa sana ya kufanya kazi pamoja na kiongozi kama huyo kwa sababu naamini yale anayoamini yeye… naweza kuwa askari mzuri wa kufanya naye kazi,” aliongeza Madaraka.
Mbunge wa jimbo la Butiama aliyemaliza muda wake ni Nimrod Mkono (CCM). Alisema akibahatika kupewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM atakuwa chachu ya kuwezesha chama hicho kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Madaraka alisema amekuwa mkazi wa jimbo la Butiama kwa miaka 20 sasa (tangu Oktoba 1999 aliporudi kumzika Mwalimu Nyerere), hivyo muda huo umemwezesha kufahamu changamoto zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.
“Hivyo nitakuwa chaguo sahihi na suluhisho sahihi kwa wakazi wa jimbo la Butiama,” alisema.
Aliweka wazi kuwa amefurahishwa na kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na CCM chini ya Mwenyekiti wake wa kitaifa, Rais Magufuli ambaye amesimamia vizuri utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho katika kuleta maendeleo Tanzania.