Magufuli: Ruksa Machinga, mama lishe, Daladala stendi mpya Dodoma “msiwarushe vichura”
0
June 18, 2020
Rais Dkt. John Magufuli ametoa agizo kwa Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, kuhakikisha wafanyabiashara ndogondogo (Machinga), mama lishe pamoja na magari ya mizunguko mifupi jijini, (Daladala) kutengewa maeneo ya kufanya kazi katika stendi mpya ya kisasa Dodoma.
Ametoa agizo hilo mapema leo, kwa njia ya simu, baada ya Mkurugenzi kuwatembelea wafanyabiashara katika stendi hiyo na kusikiliza kero zao.
Magufuli amesema “Mama lishe lazima wawepo, mimi niingie nikale chakula cha mia tano badala ya elfu tano, hayo ndiyo maisha yetu ya watanzania, lakini kieleweke hiyo stendi haikujengwa kwaajili ya matajili, nimeijenga kwaajili ya watanzania wote wakiwepo maskini”
Kwa upande wa machinga amesema ” Hakuna sababu ya kuwa na stendi ya watanzania wote wa maisha yote, halafu hao hawashiriki hata kuuza zabibu hapo”
Usafiri mwingine wa daladala na pikipiki Rais amesema ” Nilazima jiji litengeneze mazingira, watu wa daladala wawe wanaweza kufika pale, wa bodaboda waweze kufika pale, wa pikipiki waweze kufika pale, ili kusudi hata mvua ikiwa inanyesha mtu asianze kutembea na mizigo yake, wapo wengine wagonjwa..”
Aidha ametoa onyo kwa walinzi waliopewa kazi kwenye stendi hiyo kutoka Suma JKT kuacha kuwarusha watu vichura na kufanya kazi ya kuwalinda, kama wanavyofanya mikoa mingine “Hapo sio jeshini…hawakuajiliwa pale kuwapigisha vichura” Amesisitiza JPM.
Kwa upande wake Mkurugenzi, Kunambi ameahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa ndani ya muda mfupi na kuwatafutia vijana mikopo kama ambavyo Rais ameagiza.