MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa wa msimu wa kipupwe nchini, kwa Mwezi Juni hadi Agosti 2020 na kusema kuwa mwaka huu kutakuwa na vipindi vya upepo mkali wa kusi na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchini.
Pia mamlaka imesema, vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kuwepo katika msimu huu katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na na asubuhi.
Akizungumzia msimu huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi amewataka wananchi kufuatilia utabiri huo wa msimu wa kipupwe kwa kipindi cha Juni-Agosti (JJA) 2020, ambapo mvua za msimu wa Machi hadi Mei ambazo zilileta athari hapa nchini zimeisha.
Amesema athari mbali mbali zinazoweza kujitokeza ni kuongezeka kwa hali ya ukavu na upepo lakini pia inaweza kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine. Jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza hivyo wananchi pamoja na sekta mbalimbali wanapaswa kuchukua tahadhari.
Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa hasa katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Juni na kupungua kuelekea mwishoni mwa msimu yaani mwezi Agosti kwa maeneo ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma, maeneo haya yanatarajiwa yatakuwa na joto la kawaida kati ya nyuzi joto 6 na 12, hata hivyo baadhi ya maeneo hususan katika mikoa ya Njombe na Mbeya yanatarajiwa kuwa na joto la chini ya nyuzi joto 6”. alisema Dkt. Kijazi
Dkt Kijazi alielezea hali ya joto katika maeneo mengi hapa nchini, huku akibainisha kuwa joto la kawaida linatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani na kuashiria uwepo wa vipindi vichache vya baridi ikilinganishwa na hali ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya Juni-Agosti katika maeneo hayo.
Kuhusu mvua, Dkt. Kijazi amesema, vipindi vya Upepo unaovuma kutoka mashariki na kusini mashariki (Matlai) vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache
Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi alisema, vipindi vya Upepo unaovuma kutoka mashariki na kusini mashariki (Matlai) vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache