Mkuu Wa Idara Ya Habari Na Mawasilino ya mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC Haji Sunday Ramadhan Manara, amesema msimu huu kikosi chao kina uwezo wa kufikisha alama 100 na kuweka historia katika michuano ya Ligi Kuu.
Simba SC wanaongoza msimamo wa Ligi wakiwa na alama 71, na mwishoni mwa juma hili wataendelea na michezo ya ligi hiyo kwa kuwakabili Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Akizungumza kwenye kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM, Manara amesema haoni sababu ya kikosi chao kushindwa kufikisha alama 100 katika mshike mshike wa Ligi Kuu msimu huu, huku akitoa tahadhari kwa Azam FC na Young Africans kutokua na matarajio ya kubadili muelekea wa Simba SC katika ubingwa ndani ya miaka mitano hadi kumi ijayo.
Kuhusu mipango ya Simba SC upande wa Kombe La Shirikishi Tanzania Bara (ASFC), Manara amesema dhamira yao ni kutwaa ubingwa wa michuano huyo kwa kuzichapa Azam FC na Young Africans na kisha kumbanjua watakakutana naye kwenye mchezo fainali mjini Rukwa.
“Uhakika kwa Asilimia 100 naona kabisa kwa sasa tunaweza kuchukua ubingwa mara tano mfululizo, kama Azam FC hawatabadilika tutachukua ubingwa mara 10 mfululizo, Yanga hawana Ushindani.” Amesema Manara.
“Sisi Simba ndio tutachagua tucheze mchezo upi? Tunaweza kuchagua tucheze Shirikisho la Afrika kwani nani anatupangia, sisi tunataka tumfunge Azam FC alafu Yanga amfunge Kagera sugar ili tukutane nae tumalize Ubishi wa Sherehe Yao ya kila tarehe 8.”
Katika hatua nyingine Manara amewarushia dongo watani wao wa jadi Young Africans kwa kusema kikosi chao kimesafiri na basi kuelekea Shinyanga, ambapo watacheza na Mwadui FC keshokutwa Jumamosi.
“Timu kubwa inasafiri kwa gari mwisho kilometa 300, sio wanasafiri kwa gari hadi Shinyanga. Watu wapite Itigi wale ubwabwa au nzega wanunue magimbi na mahindi ya kuchemsha”
Pia akazungumzia upande wa usajili ambao wanatarajia kuufanya wakati wa dirisha kubwa, mara baada ya kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Manara amegusia usajili huku akikumbushia kauli iliyotolewa na muwekezaji na mwenyekiti wa bodi ya Simba SC Mohamed Dewji, kwa kuwatoa hofu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Mohammed Dewji ‘MO’ aliwahakikishia mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa wamepanga kutomuachia mchezaji yeyote katika dirisha kubwa la usajili la kiangazi lakini pia watamchukua mchezaji yeyote wanayemtaka kama kocha anamwitaji.
“MO” ni Mwanafasihi, unahitaji kuwa na akili kubwa kumuelewa na ndo maana akasema yeye atasajili yeyote endapo kocha atamuhitaji Na kocha hawezi muhitaji Lionel Messi Bali ndani ya Afrika au nchini”
“Ninaposema tutafyatua mioyo ya watu kwenye usajili sio kumsajili mchezaji wa Yanga, wachezaji tutakaoshusha ni wa level za kushindana na klabu kubwa Afrika” Maneno Ya Afisa Habari Wa Klabu Ya Simba Sc Haji Manara.