Mkuu wa NATO Apuuzia Kitisho cha Marekani Kuondosha Haraka Wanajeshi wake Ujerumani
0
June 17, 2020
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amepuuzia kitisho cha Marekani kuharakisha kuondosha maelfu ya wanajeshi wake nchini Ujerumani, akisema serikali mjini Washington bado haijafanya maamuzi ya mwisho juu ya lini na vipi hatua hiyo itatekelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa ulinzi wa jumuiya hiyo, Stoltenberg amesema suala hilo litajadiliwa kwenye mkutano huo, na pia amewasiliana na pande zote mbili, Marekani na Ujerumani.
Rais Trump alisema hapo jana kwamba anaamuru kuondolewa kwa kiwango kikumbwa cha wanajeshi wa nchi yake waliopo Ujerumani, kutoka 34,500 waliopo sasa hadi 25,000. Hata hivyo, wajumbe wa chama chake mwenyewe cha Republican wamemkosowa vikali kwa uamuzi huo, wakisema ni kama kuipa zawadi ya bure Urusi na pia kutishia usalama wa taifa la Marekani.
Ujerumani ni kituo kikubwa kwa operesheni za kijeshi za Marekani katika Mashariki ya Kati na ni makao makuu ya kamandi ya jeshi la Marekani barani Ulaya.
Tags