Mauaji hayo yametokea wakati polisi walipokuwa wakijaribu kumfanyia kipimo cha kubaini iwapo alikuwa ametumia mihadarati. Polisi mjini Atlanta wamesema kwenye purukushani hiyo mwanaume huyo Rayshad Brooks aliinyakua bastola ya kutia ganzi kutoka kwa polisi ambaye alimpiga risasi wakati alipokuwa anakimbia.
Mauaji ya Brooks aliyekuwa na umri wa miaka 27 yamechochea wimbi jipya la maandamano mjini Atlanta, baada ya lile la maandamano ya kupinga kifo cha George Floyd aliyeuawa mjini Minneapolis ambayo kwa sasa yamepungua kasi nchini Marekani na duniani kote.
Meya wa Atlanta Keisha Lance Bottoms alitangaza kujiuzulu kwa mkuu huyo wa polisi kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati watu wapatao 150 walipoandamana nje ya mgahawa wa Wendy ambako kijana huyo aliuawa siku ya Ijumaa jioni. Meya huyo alitoa wito wa kufutwa kazi mara moja afisa wa polisi aliyemfyatulia risasi Rayshad Brooks.
Meya huyo ameeleza kuwa hatua ya kujiuzulu kwa mkuu wa polisi wa jiji la Atlanta ni uamuzi wake binafsi na kwamba mkuu mwandamizi wa idara ya kurekebisha tabia Rodney Bryant atakaimu nafasi hiyo kwa muda hadi pale mkuu mpya wa polisi atakapopatikana.
Taarifa ya Polisi wanaoendesha uchunguzi
Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya uchunguzi ya Georgia, inayochunguza mauaji hayo, malumbano yalianza baada ya maafisa wa polisi kupokea malalamiko ya kuwa palikuwa na mtu aliyekuwa amelala ndani ya gari lililoegeshwa kwenye njia kuelekea kwenye mgahawa wa Wendy. Ofisi hiyo ya uchunguzi GBI imeeleza kwamba majibu ya Brooks baada ya kupimwa yalionyesha kuwa alikuwa ametumia mihadrati lakini akakaidi pale polisi walipotaka kumtia mbaroni.
Mkurugenzi wa GBI Vic Reymonds ameeleza kwamba hapo ndipo Brooks aliponyakua bastola ya kutia ganzi kutoka kwa polisi mmoja na kuanza kukimbia tukio lililosababisha polisi huyo kumfyatulia risasi mara tatu.
Tamko la wakili wa familia ya Brooks
Lakini wakili wa familia ya marehemu Brooks bwana Chris Stewart, amepinga vikali madai ya polisi na amesisitiza kwamba afisa aliyempiga risasi Brooks ashtakiwe kwa kusababisha kifo kutokana na kutumia nguvu bila sababu. Amesema hakuna njia mbili katika utekelezaji wa sheria, yaani upande mmoja bastola ya kutia ganzi kuwa ni silaha isiyoleta madhara lakini wakati huo huo kwa sababu ni mtu mweusi aliyeichukua na kuanza kukimbia bastola hiyo igeuke na kuwa silaha ya hatari na kumfanya polisi atoe bunduki na kumfyatulia risasi mtu huyo.
Waandamanaji pamoja na wanafamilia ya Brooks, walikusanyika siku ya Jumamosi nje ya mgahawa alikouawa Brooks kwa kupigwa risasi. Waliutia moto mgahawa huo na kuifunga baraara kuu ya mjini Atlanta. Kati ya waandamanaji hao alikuwepo Crystal Brooks, shemeji yake Rayshard Brooks ambaye amesema Brooks hakumsumbua wa kumdhuru mtu yeyote, bali polisi walikwenda kwenye gari lake lililokuwa limeegeshwa na walimtoa nje ya gari na kuanza kugombana naye. Marehemu Brooks alifariki katika hospitali moja ya mjini Atlanta alikopelekwa baada ya kupigwa risasi.