Molinga Atoa Kauli ya Kutisha Yanga SC


STRAIKA mbabe wa Yanga, David Molinga ‘Falcao’, amesema kuwa mwishoni mwa msimu huu ataachana na klabu yake hiyo ya sasa na anatarajia kwenda kujiunga na Klabu ya Renaissance Sportive ya Morocco ila anaamini watamkumbuka.

Hadi sasa Molinga ndiye kinara wa mabao ndani ya Yanga, ambapo ameshaifungia klabu hiyo mabao 10 kwenye Ligi Kuu Bara, japo mashabiki na mabosi wa timu hiyo wameendelea kutoridhishwa na uwezo wake.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Molinga alisema tangu alipotua Yanga alikuwa akitamani sana siku moja kuondoka akiwa mfungaji bora wa ligi, lakini anaona uvumilivu umekuwa mdogo kwao hivyo kwa sasa anafikiria kwenda Morocco kujaribu bahati yake.



“Siyo kwamba mimi sina uwezo wa kuwa mfungaji bora kwenye ligi hii, ila kinachonisumbua ni suala la kuwa nje kwa muda mrefu jambo ambalo wengi hawataki kulikubali na kunipa muda, nimecheza timu nyingi kubwa ila niliumia na hiyo ndiyo sababu ya kupungua uwezo.

 

“Kama ningepata nafasi ya kuchezea Yanga tena msimu ujao basi naamini ningeweza kupata utimamu mzuri na hakika Yanga wangefurahia.“Kwa sasa acha niondoke ila najua watakuja kunikumbuka maana ninakoenda nitapata muda mzuri wa kujiweka fiti na kufunga,” alisema Molinga.Ameeleza kuwa ameshasaini mkataba wa awali wa miaka mitatu kujiunga na timu hiyo ya Morocco kwa kuwa mkataba wake na Yanga unaelekea ukingoni.

 

“Unajua mimi sikusafiri kipindi cha Corona kwa kuwa Yanga walitaka kuzungumza na mimi kuhusu mkataba wangu, lakini haikuwa hivyo.

 

“Mara kadhaa imewahi kujitokeza nikiwakumbusha viongozi kuhusu mkataba wangu lakini nikawa nazungushwa tu, hivyo sikujua hatima yangu, mwisho nikachoka, nikaamua kusaini hiyo timu ya Morocco mkataba wa awali ambapo rasmi nitajiunga nao baada ya msimu huu.

 

“Sheria ya Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) zimeeleza kuwa kutokana na Corona tunalazimika kumalizia msimu kwa muda uliosalia kisha ndio tutaondoka kwenda klabu nyingine kwa wale wanaohitaji kuhama.

 

AKATAA FEDHA ZA YANGA SC

Mara baada ya mchezo wa juzi Mcongo huyo alionyesha jeuri baada ya kukataa fedha alizokuwa akitupiwa na mashabiki wa timu yake kwa kufunga mabao mawili dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika Ligi Kuu Bara.

 

Molinga aliingia akitokea benchi akichukua nafasi ya kiungo Mapinduzi Balama na kufunga mabao hayo ambayo yaliamsha shangwe nyingi kwa Wanayanga uwanjani hapo kwa kuwa awali walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 80.

 

Baada ya mchezo alipokaribia mlango mkubwa wa kuingilia wachezaji, alikutana na shangwe kubwa la mashabiki waliokuwa wakimsubiria kwa ajili ya kumtunza fedha ambazo alizikataa na kuingia vyumbani.

 

“Molinga katuthibitishia ubora wake katika mchezo huu, kiukweli amefunga mabao muhimu na kutupatia pointi moja, tunashindwa kuelewa sababu za yeye kuanzia benchi ni nini wakati ana uwezo mkubwa wa kufunga kama leo (jana) ilibakia kidogo tudharirike,” walisikika mashabiki wa Yanga.

 

Kuhusu hicho kilichotokea, Molinga anasema: “Sikutaka fedha zao kwa kuwa nafanya hii kazi kwa mapenzi yangu, kuna muda (mashabiki) hawaeleweki, unapokuwa kwenye hali ngumu lazima wakuelewe.

 

“Sikutaka fedha wala mazungumzo nao ili wajifunze kuwa hata sisi wachezaji huwa tunaumia wanapotutukana tusipopata matokeo mazuri.”


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad