Mwanasayansi wa Iran, Majid Taheri amerejea nyumbani leo baada ya kuachiwa kutoka gerezani nchini Marekani, kama sehemu ya kubadilishana wafungwa.
Shirika la habari la Iran, ISNA limeripoti kuwa baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Imam Khomeini, Taheri alilakiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Jaberi Ansari.
Mwanasayansi huyo aliyekuwa anashikiliwa nchini Marekani kwa miezi 16, aliachiwa huru Alhamisi iliyopita, wakati ambapo Iran ilimuachia huru veterani wa kikosi cha jeshi la majini la Marekani, Michael White.
Taheri ni mwanasayansi wa pili kurejea Iran kutoka Marekani, baada ya wiki iliyopita Cyrus Asgari kurejea pia nyumbani.
Taheri amekuwa akishutumiwa kukiuka vikwazo vya Marekani na mwezi Desemba alikiri kukiuka ripoti za kifedha kwa kuweka benki dola 277,344. Hata hivyo, Taheri amekanusha madai dhidi yake, akiyaita ni ya ''uongo na yasio sawa''.