Mwizi Aliyesinzia Ndani ya GARI Baada ya Kuiba Shekhe Atoboa Siri


SHEHE Ahmed Kandauma wa Taasisi ya Kiislam ya Irshaad ya jijini Dar es Salaam, amejitokeza na kulitobolea siri tukio la mtu anayedaiwa ni mwizi kusinzia muda mfupi baada ya kuiba nyumbani kwa mwandishi wa habari Farouk Karim wa Visiwani Zanzibar.

Mwandishi huyo alidai kuwa usiku wa kuamkia Juni 2, mwaka huu mtuhumiwa huyo aliingia nyumbani kwake kwa lengo la kuiba, lakini hakufanikiwa kutoka eneo la tukio baada ya kupitiwa na usingizi mzito, kisha asubuhi kunaswa kirahisi. Jambo ambalo limewafanya baadhi ya watu kupigwa na butwaa.

SIKIA MADAI YA MWANDISHI

“Huyu mwizi (kwetu haya ni madai) kaingia usiku wa manane, karuka geti na hatuna mlinzi pale nyumbani. “Kakusanya nguo zilizokuwa zimeanikwa, kaziweka kwenye mfuko. katika magari yaliyokuwepo pale, gari moja ilikuwa wazi, kaingia kupitia mlango wa abiria.

“Akaenda upande wa dereva, akachukua power window ya gari ikamshinda na ndipo akalala hapohapo. Tumempeleka polisi kama ambavyo huwa tunamsindikiza bi harusi. “Ile kulala, huenda kaiba sana karidhika, na dawa kubwa ya kumfanya mwizi alale ni moja tu, kuomba Mungu akulinde wewe na nyumba yako na watu kama sisi ambao hatuna madhambi, dua zinakubaliwa…” alisema Farouk.

SHEHE ATOBOA SIRI

Baada ya mwandishi huyo kudai kuwa ni mtu asiyekuwa na dhambi na hivyo anao uwezo wa kuomba dua ya kumnasa mtu mbaya, Amani lilimtafuta shehe Kandauma ili kupata maoni yake juu ya tukio hilo. “Hilo linawezekana na dua hizo zipo, lakini inahitajika huyo anayeomba awe mcha Mungu wa daraja la juu sana.

“Hivihivi haiwezekani jambo hilo kutokea, maana matego ya namna hiyo yako ya aina nyingi, kuna hayo ya wacha Mungu na mengine ni ya kishirikina. “Nakumbuka kuna kisa kimoja kilimtokea Mtume Muhamad ‘SAW’ alipokuwa akitoka Makha kwenda Madina.

“Usiku wa kuamkia safari yake, watu 40 wabaya waliizingira nyumba yake kwa lengo la kumuua, lakini yeye kwa kulitambua hilo, alianza kuomba dua kisha akateka mchanga na kuwamwagia watu hao. “Basi wote walipigwa bumbuwazi na mtume alitoka salama kuelekea Mji wa Madina, lakini kama nilivyosema, utakatifu ni jambo la kwanza kabisa kabla ya dua kufanyika,” alisema shehe Kandauma.



UTAKATIFU WA MWANDISHI WAGEUKA GUMZO

Hata hivyo, gumzo kubwa baada ya tukio hilo la Zanzibar, lilikuwa kwenye kauli aliyoitoa mwandishi Farouk ya kusema kuwa “Hana madhambi” ambapo wengi walihoji “Ni kweli ana huo utakatifu wa daraja la juu unaosemwa au kuna njia nyingine ametumia?”

Kwa mujibu wa maandiko, suala la utakatifu ni kati ya mtu na Mungu ambaye ndiye mhukumu mkuu wa wanadamu wote.

KUTAFUTA KIKI KWATAJWA

Katika hatua nyingine, baadhi ya watu walisema kwenye mitandao ya kijamii kuwa, huwenda tukio hilo ni la kutengeneza ili kumpatia kiki mwandishi huyo au mtu wake wa karibu.

“Inawezekana jamaa kapata mashehe wetu wa mtaani, sasa wanataka kupiga hela, wameona ni vyema watengeneze tukio ili kuvuta watu.

“Kwenye mazungumzo yake Farouk ni kama amesema wanaotaka dua hiyo wamtafute, sasa na yeye amekuwa shehe au ndiyo kafikia daraja la kuombea watu dua nzito kama hizo, mimi hata sielewi,” mtu mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram ambako picha za tukio zilipostiwa.

UTHIBITISHO WA POLISI WAKOSEKANA

Pamoja na kuelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alichukuliwa na polisi baada ya kuamshwa kwa kunaswa vibao vitatu, Amani limeshindwa kuzipata mamlaka za polisi kuweza kulizungumzia tukio hilo na ukweli zaidi kupatikana.

Stori: Memorise Richard, Amani

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad