WAZIRI Mkuu Mstaafu ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, ametaja mikakati 11 ya ushindi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kutokana na na hali hiyo ameiagiza Kamati ya Siasa ya mkoa huo, kuhakikisha inatatua na kumaliza migogoro yote ya kisiasa ndani ya chama hicho ikiwamo ile ya viongozi.
Hayo aliyasema jana jijini hapa, wakati akifungua kikao cha Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma, ambapo alisema kuwa CCM kimeandaa mikakati 11 ya kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu kwa asilimia 100.
Alisema kuelekea Uchaguzi Mkuu kati CCM haiku tayari kuona migogoro ndani ya chama hivyo ni lazima wahakikishe wanasafisha sambamba na kuvunja makundi yote ya ndani.
Alisema migogoro inaweza kuwa kwa viongozi ndani ya chama, unakuta Mwenyekiti wa chama wa mkoa ndani ya kamati ya siasa yenyewe hawaelewani.
“Kama hamuelewani kamati ya siasa mkoa mtatuongoza namna gani sisi wengine, ukipata kitu kama hicho lazima utafute mbinu za haraka kukimaliza,”alisema.
Alisema, migogoro, ya siasa ndani ya chama ambayo inatokea miongozi mwa viongozi, haiwezi kuwapeleka mahali pazuri na badala yake itawavuruga katika uchaguzi,
“Sina mashaka kama tutakamilisha mikakati tuliyojiwekea ni dhahiri kuwa ushindi upo, mara zote tulipokuwa tunaelekea katika uchaguzi mkuu, kigezo kilichokuwa kinatusaidia katika kuelekea uchaguzi unafuta ilikuwa ni matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Ndiyo tulikuwa tunaanzia pale na kwa kadri tutakavyokuwa tumeshinda ngazi ya vitongoji, vijiji mana yake ni kwamba chama ngazi ya matawi na mashina imefanya kazi vizuri, ndio mana mnaona ushindi wa mwaka 2015 kwa upande wa Dodoma ilikuwa ni mtikisiko mzuri,” alisema.
Alisema, katika mikakati ambayo ni lazima waweke msisitizo mkubwa ni suala la kuimarisha mashina na matawi kwa sababu huko ndiko wapiga kura walipo.
“Jitihada za chama, kutupa macho kwenye ngazi za mashina na matawi ziendelea kupewa mkazo mkubwa hata ikilazimika kuzunguka nyumba kwa nyumba na kuomba kura tutafanya mana ndio namna ya kutafuta kura katika ngazi ya chini,”alisema.