Polisi na Wenzake Wanne Mbaroni kwa Tuhuma za Mauaji Mbeya
0
June 23, 2020
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne akiwemo Askari Polisi mmoja namba G.8695 PC JOHN KAIJAGE [34] Mkazi wa Isyesye Jijini Mbeya, FOTUNATUS KAGANDE [23] Mkazi wa Iwambi, PETSON DANIEL [22] Mkazi wa Iwambi na JASTINI KAGANDE [27] Mwanafunzi St.John na Mkazi wa Iwambi kwa tuhuma za kumuua ERASTO MWALWEGO [29] Dereva Pikipiki @ Bodaboda na Mkazi wa Nzovwe.
Ni kwamba mnamo tarehe 20.06.2020 majira ya saa 21:00 Usiku huko katika nyumba ya kulala wageni iitwayo “The Governor City Lodge” iliyopo Iwambi Jijini Mbeya watuhumiwa walimshambulia ERASTO MWALWEGO [29] Dereva Pikipiki @ Bodaboda na Mkazi wa Nzovwe sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kitu butu.
Mhanga alipelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu na mnamo tarehe 21.06.2020 majira ya saa 06:00 Asubuhi alifariki akipatiwa matibabu. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
KUGHUSHI NYARAKA YA SERIKALI.
Mnamo tarehe 21.06.2020 majira ya saa 14:30 Mchana huko Kijiji cha Kilwa kilichopo Kata ya Kajunjumele, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata BAHATI CHARLES NDINAGWE [21], Mkazi wa Kilwa – Kajunjumele akiwa na barua ya kughushi inayoonyesha kuwa imetoka katika Ofisi ya Usalama wa Taifa Makao Makuu kwenda kwa mtuhumiwa huyo ikimjulisha kuwa ameteuliwa kujiunga na idara hiyo ya Usalama wa Taifa. Kiini ni kutaka kupata ajira. Mbinu ni kuchapa barua hiyo kwa namna inayofanana na barua za idara hiyo. Ufuatiliaji unaendelea.
KUPATIKANA NA POMBE KALI ZILIZO PIGWA MARUFUKU NCHINI.
Mnamo tarehe 19.06.2020 majira ya saa 19:30 Usiku huko maeneo ya Ushuru na Forodha, Kata ya Njisi, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata HANSI ERASTO [38] Mkazi wa Njisi akiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku nchini aina ya “ice” boksi 02, “right choice” boksi 01 na “figter vodco” boksi 02 kutoka nchini Malawi.
KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Mnamo tarehe 19.06.2020 majira ya saa 14:00 Mchana huko kizuizi cha Kayuki, Kijiji na Kata ya Ilima, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, katika barabara Kyela – Tukuyu tuliwakamata MARIAM MUSTAFA [40] mkazi wa Usangu – Rujewa akiwa na vitenge doti 5, MESIA RAMADHANI [25], mfanyabiashara na mkazi wa Sumbawanga akiwa na vitenge doti 42, JANETH JACKSON MWANSITE [40] mkazi wa Uyole akiwa na vitenge doti 12 na HAWA KIBONA [24] mfanyabiashara na mkazi wa Mbozi akiwa na vitenge doti 25 kutoka nchini Malawi. Taratibu za kiforodha zinafanyika.
Tags