Sharon “Nikila Sabuni Napata Raha, Hasa Arangi, Maombi Hayajanisaidia”


Kwa kawaida, sabuni hutumiwa kusafisha vitu mbalimbali. Huwekwa mbali na chakula, na ikitokea kwamba chakula chako kiingiwe na sabuni hautakila tena.


Lakini wanawake wawili katika familia moja eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya wamekuwa na uraibu wa ajabu sana, kwao sabuni imekuwa ndiyo chakula wakipendacho mno.

“Hakuna kitu kinachonipa raha zaidi kama wakati ninapoanza kula sabuni. Siwezi kuelezea utamu ninaouhisi ninapoonja kipande cha kwanza cha sabuni. Hufurahia zaidi sabuni ya rangi, kwangu ndiyo huwa tamu kuliko vitu vingine vyote,” anasema mmoja wao Sharon Chepchirchir.

Sharon Jepchirchir, 25, na dada yake Lydia Chepkemboi mwenye umri wa miaka 18 wamekuwa na uraibu huu kwa muda mrefu na kuwaacha wanakijiji vinywa wazi.

Mabinti kutoka kijiji cha Kiboji, eneo la Mosop, wanasema kuwa kuanzia machweo, hamu kubwa ya kula sabuni huanza.

Kwa hivyo, kabla ya kula au kunywa kitu kingine chochote, ni lazima waanze na kula vipande vya sabuni. Ni kama kiamsha kinywa kwao.

Kufikia jioni, wanakadiria kwamba huwa wametafuna na kumaliza mti mzima wa sabuni ya kipande.

Wanasema kuwa hawapendi tabia walio nayo lakini wameshindwa kujizuia.Sharon JepchirchirSharon Jepchirchir akionesha umahiri wake wa kula sabuni

Kuiba sabuni
Sharon anasema licha ya kuchukua hatua za kujiwekea masharti mapya ya kuachana na tabia hiyo, yeye hujipata na njaa isiyoeleweka na kuanza kula sabuni tena.

“Jambo hili ni la ajabu sana hata kwangu mimi, imenifanya niwe na tabia ya kuiba sabuni nyumbani hadi imefikia kiwango cha mama yetu kuficha sabuni ya aina yoyote. Anafahamu kuwa tukiipata tunaanza kuila,” Sharon alisema.

Kulingana na Sharon, tabia hii alianza wakati alipokuwa na miaka mitano. Dadake mdogo alianza tabia hiyo akiwa bado mchanga.Kina dada wanaokula sabuni na mama yao (kulia)Sharon Jepchirchir (Kushoto) dada yake mdogo Lydia Chepkemboi (Katikati) na mama yao (kulia)

Mama wa mabinti hawa wawili pia amekuwa na mawazo mengi kuhusiana na tabia hii ya ajabu ya wanawe.

Sharon anasema kuwa hakuna maombi na matambiko ambayo hawajafanyiwa katika juhudi za kucha tabia hii.

“Tumefanyiwa maombi na kupakwa hata mafuta ya upako. Kwa wiki kama mbili hivi itaonekana kana kwamba tumeacha tabia hii, lakini hamu na tamaa ya sabuni hurejea hata maradufu kuliko ilivyokuwa,” Sharon alisema

Kwa kuwa tabia hii imeanza kuwa na kero hasa kwa mama yao, mabinti hawa wamejifunza kujificha sehemu mbalimbali ili kuendeleza uraibu wao.Lydia ChepkemboiLydia Chepkemboi (Kulia) akila sabuni

Kwa siku Sharon anasema kuwa wanaweza kula sabuni hata kwa mara tano.

Sababu ya uraibu wao ni nini?
Sharon anasema walipoangaziwa na vyombo vya habari nchini Kenya walienda hospitali kufanyiwa utafiti wa kubaini kwa nini wanakula sabuni.

Sharon anasema kuwa matokeo ya utafiti wa kwanza yalionyesha kuwa kina dada hao wawili wana upungufu wa madini ya chuma (iron) kwenye miili yao. Aidha, wana tatizo la kuwa na kiwango kidogo cha damu mwilini.

Kwa hivyo ile njaa na hamu ya kula sabuni kila wakati inatokana na ukosefu wa madini hayo muhimu.

Vipimo vya damu wakati wa utafiti huo ambao ulifanywa mwaka jana vinaonyesha kuwa kiwango chao cha damu kilikuwa painti 7 , ilhali mwili wa binadamu unahitaji kati ya painti 14 na 18.

Vile vile seli za damu za miili yao zinaonekana kuwa ndogo mno kuliko za kawaida.

“Kupitia matokeo tuliyofanyiwa pia iligundulika kuwa mmoja wetu hana madini ya chuma kabisa, na hicho ni kitu cha ajabu mno,” Sharon aliongeza.Kina dada wanaokula sabuniSharon Jepchirchir (kushoto) dada yake mdogo Lydia Chepkemboi (kulia)

Sabuni inasaidia mwili na chochote?
Wakati Sharon na Lydia walipofanyiwa uchunguzi madaktari walikuwa wanadhania kuwa huenda mabinti hawa wanakosa kemikali aina ya sodium na potassium katika miili wao, na huenda ndiyo sababu kuu yao kuwa na njaa ya sabuni.

Sabuni huundwa kwa mchanganyiko wa kemikali ikiwemo zile za sodium na pottasium, pamoja na tindikali. Kwa hivyo, kulingana na wataalam, sabuni haina manufaa yoyote kwa mwili wa binadamu ila inaweza kuwa na madhara.

Na huenda kuna hatari ya kula sabuni ambayo ina rangi na manukato kwani zile kemikali za kuongeza rangi na manukato zinaweza kudhuru mwili wa binadamu.

Kibarua kwa wanasayansi
Sasa kibarua kigumu kwa wataalamu katika kuifahamu vyema hali ya Sharon na Lydia kimekuwa ni kutafuta ni kwa nini mabinti hawa hawana madini ya iron na pia ukosefu wa damu mwilini.

Kwa kuwa Sharon na Lydia wote ni watu wanaokula chakula chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini, Sharon anasema pengine miili yao haina uwezo wa kuhifadhi madini hayo. Madini hayo hupita tu mwilini.

“Ni jambo linalosikitisha sana. Nashangaa ni kwa nini mimi na dadangu tuna tabia hii. Mbona hata matabibu wenyewe wameshindwa kung’amua `tatizo letu , ambalo linatuweka kwenye aibu kuu kila siku ?” anashangaa Sharon

Wasiwasi wa Sharon umekuwa onyo walilopewa kwamba wakiendelea kula sabuni wanaweza kudhuru miili yao na maisha yao ya baadaye.

Sharon ambaye tayari ana mchumba, anasema kuwa ni aibu unapokuwa karibu na mpenzi wako na huku unanuka sabuni mdomoni.

Ingawa anasema kuwa amemueleza wake wa moyoni kuhusu uraibu huu alionao ambao sio wa kawaida, Sharon anasema kuwa anajua moyoni mwake ni kitu ambacho kinamsumbua mpenzi wake. Lakini nguvu ya kuacha tabia hii hana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad