Simba Yaipiga 3-0 Mwadui FC Uwanja wa Taifa
0
June 20, 2020
MABAO ya Hassan Dilunga na Augustino Samson ambaye amejifunga, yametosha kuipa Simba SC uongozi dhidi ya Mwadui FC katika dakika 45 za kipindi cha kwanza kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ingawa hadi sasa inaongoza kwa mabao 3-0
Simba ambao kikosi chao cha kwanza kilikuwa na mabadiliko kadhaa ukilinganisha na kile ambacho kilianza katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting, walionekana kuanza kwa kasi kipindi hicho cha kwanza.
Huku wakionekana kuwa na nguvu kubwa katika maeneo yao ya pembeni ambayo walikuwa wakicheza kwa upande wa kulia Shomari Kapombe na kushoto, Mohammed Hussein maarufu kama ‘Tshabalala’.
Dakika ya tisa tu ya kipindi cha kwanza, Simba walijipatia bao la kwanza kupitia kwa Dilunga baada ya kazi nzuri ya Bocco ambaye alimtengenezea. Bocco leo ameanza mwenyewe katika safu ya ushambuliaji ya Simba tofauti na mchezo uliopita ambapo alicheza na Meddie Kagere.
Wakiwa na mabeki watatu wa kati ambao ni Pascal Wawa, Erasto Nyoni na Kennedy Juma ilikuwa rahisi kwa Kapombe na Tshabalala kupanda na kushuka katika staili ya kisasa ambayo huitwa kama ‘Wing Backs’.
Gerald Mdamu na Raphael Aloba ambao wamekuwa wakitegemewa na Mwadui katika safu yao ya ushambuliaji walishindwa kufua dafu mbele ya ukuta wa Simba.
Simba ilijipatia bao la pili dakika ya 21 baada ya Samson kujifunga kutokana na presha ya shambulio ambalo wekundu wa Msimbazi walilifanya, ilikuwa ni pasi ya Kapombe aliyekuwa akiipenyeza ndani ambayo beki huyo alikutana nayo na kujikuta anamfunga kipa wake, Mahmoud Amir.
Karibu dakika zote za kipindi cha kwanza Simba walionekana kutawala huku wakipoteza nafasi kadhaa za wazi katika eneo la kiungo walicheza Said Ndemla, Gerson Fraga, Hassan Dilunga na Luis Miquissone.
Dilunga na Miquissone muda mwingine walikuwa wakitanua katika maeneo ya pembeni ambayo walikuwa wakionekana, Kapombe na Tshabalala wakicheza vizuri.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kupata bao la tatu kupitia kwa John Bocco aliyeunganisha kwa kichwa mpira uliogonga mwamba baada ya shuti la Miquissone
Tags