TAKUKURU Manyara yawakamata watumishi watatu wa TRA kwa kuomba Rushwa





Na John Walter-Manyara. 

Ikiwa ni wiki mbili tu kupita tangu Maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato mkoani Manyara kukamatwa na TAKUKURU  kwa tuhuma za  kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi Milioni kumi kwa mfanyabiashara wilayani Mbulu, wengine watatu wamekamatwa kwa makosa kama hayo. 

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara Holle Mkungu amesema kwa sasa wanawashikilia maafisa watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani hapo kwa tuhuma za kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi Milioni moja kutoka wa mfanyabiashara wilayani Babati.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo June 12,2020, Makungu amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Jackline Leonard Manjira, Joseph Mtandika na Ephrahim John Medard ambao waliomba rushwa hiyo kutoka kwa mfanyabiashara wa duka la reja reja ili wasimuongezee makadirio ya kodi katika biashara yake. 

Uchunguzi wa TAKUKURU umebaini kwamba mfanyabiashara huyo alikadiriwa kulipa kodi ya shilingi laki mbili na nusu kwa mwaka na mtumishi wa TRA ambaye hakumdai rushwa. 

Makungu amesema mfanyabiashara huyo akaomba kulipa kodi hiyo kwa awamu na akakubaliwa ambapo mpaka mwezi Juni 2020, tayari alikuwa ameshalipa awamu ya kwanza ya kodi aliyokuwa amekadiriwa. 

Ameeleza kuwa wakati akiendelea na biashara yake huku akisubiri kulipa awamu ya pili,alifuatwa tena na watuhumiwa ambao ni Maafisa wa Mamlaka ya Mapato na kuelezwa kuwa amekadiriwa chini ya kiwango na kwamba kwa biashara yake alitakiwa kuwa na EFD Mashine na hivyo ametenda kosa. 

Ameendelea kueleza kuwa baada ya maelezo hayo walimtaka aende ofisi za TRA zilizopo mjini Babati kwa hatua zaidi ambapo aliitikia wito huo na alipofika ofisini hapo akaelezwa kuwa alikadiriwa chini ya kiwango hivyo anatakiwa kulipa kodi ya shilingi laki nne na nusu kwa mwaka na faini ya shilingi milioni tatu kwa kutotumia mashine ya EFD. 

Makungu amewaambia waandishi wa habari kuwa, mfanyabiashara huyo aliwaeleza maafisa hao kuwa hawezi kulipa fedha hizo kutokana na biashara aliyonayo vinginevyo ni bora afunge tu biashara hiyo, ambapo baada ya kutoa uamuzi huo ndipo alipofahamishwa na afisa  Jackline Manjira wa TRA Babati ili  asipigwe faini hiyo awapelekee shilingi milioni moja. 

Mkuu wa TAKUKURU ameeleza kuwa kutokana na mwamko walionao wananchi wa Manyara kwa sasa,mfanyabiashara huyo aliamua kutoa taarifa TAKUKURU na mtego wa shilingi Milioni moja uliandaliwa ambao uliwezesha kukamatwa kwa watumishi hao. 

Amesema uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa baada ya watumishi hao kukabidhiwa fedha za mtego wa hongo,Jackline Manjira na Eva Mtandika waliandika kwenye faili la mfanyabiashara huyo kuonyesha kuwa amesamehewa ongezeko la kodi na uamuzi wa mashine ya EFD hadi mwaka 2021. 

Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara uchunguzi utakapokamilika huku akitoa wito kwa wakazi wa Manyara na watumishi wa Umma kuwa uadilifu sio karama au kipaji ni uamuzi wa mtu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad