Vodacom Kuanza Kurusha Hadithi Za Shigongo



Mkurugenzi wa Global Publishers na mtunzi mahiri wa riwaya Afrika Mashariki na Kati, Eric Shigongo.

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Global Publishers wamezindua huduma mpya ijulikanayo kama ‘HADITHI ZA SHIGONGO’ ambayo itapatikana kupitia kipengele cha VODACOM HADITHI kupitia namba 0901767676.

Mkurugenzi wa Huduma za Kidijitali wa Vodacom, Nguvu Kamando alisema kwa kutambua umuhimu wa huduma za kidijitali, Vodacom imeungana na mtunzi mahiri wa riwaya mbalimbali za kusisimua na kuelimisha, Eric Shigongo ili kuwapatia wateja wa Vodacom hadithi mbalimbali kupitia huduma hiyo.


Kamando alisema,“Tunaamini muungano huu kati ya Vodacom, Global Publishers na kampuni ya teknohama ya Premier Mobile Solutions, utaleta huduma bora kabisa kwa mteja wa Vodacom, tukianza na hadithi na simulizi mbalimbali na baadaye tutakuwa na huduma nyingine za kuelimisha na kuburudisha jamii kwa jumla”.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Global Publishers na mtunzi mahiri wa riwaya Afrika Mashariki na Kati, Eric Shigongo, alisema:

“Kwa zaidi ya miaka 22 sasa nimekuwa nikiandika vitabu vingi na riwaya nyingi ambazo zimesomwa na Watanzania wengi. Kwa sababu watu wengi wana majukumu mengi, wanapenda kusoma riwaya zangu lakini wanakosa muda wa kukaa chini na kusoma, kwa kushirikiana na Vodacom tunakujia na utaratibu mpya wa kurekodi vitabu vyote kwa mfumo wa sauti. Sasa utaweza kusikiliza hadithi ukiwa mahali popote kwa kutumia simu yako.


Mkurugenzi wa Huduma za Kidijitali wa Vodacom, Nguvu Kamando (kushoto) akiongea jambo.

“Kwa kuanzia, tumeanza na hadithi nzuri ya kusisimua ya Damu na Machozi, ambayo inakueleza kuhusu mapambano katika maisha, machozi na damu zinazomwagika wakati wa mapambano hayo mpaka mtu anapofikia mafanikio. Ni matumaini yangu kwamba utaburudika vya kutosha.” alisema

Naye, Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho alisema: “Tunaamini ubunifu huu mahiri kutoka kwa Vodacom Tanzania wa kuhamisha riwaya mbalimbali za vitabu kuwa katika mfumo wa sauti, utasaidia kuwafikia wateja wengi wa Vodacom nchini, wateja hawa walikuwa na kiu ya kusoma hadithi za Shigongo kwa siku nyingi, lakini sasa wanaweza kusikiliza hadithi hizi kutoka kwenye simu zao za mkononi”.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma hii mpya, Kamando alisema huduma hii imetengenezwa mahususi kwa kuzingatia hali ya kipato cha Mtanzania. Mteja wa Vodacom ana uwezo wa kujiunga kwa siku au wiki au kununua kifurushi cha kusikiliza hadithi zote zinazopatikana katika huduma hii ya VODACOM HADITHI.

Kuhusu kujiunga na huduma hii, Kamando alisema: “Mteja wa Vodacom anaweza kujiunga kwa njia mbili, ya kwanza ni kwa kupiga namba 0901767676 na kufuata maelekezo au njia ya pili mteja anaweza kutuma neno SHIGONGO kwenda namba 15460. Mteja akishajiunga atapokea ujumbe wa uthibitisho na kulipia Tsh 100/= kwa siku kwa huduma ya SIKU, Tsh 450/= kwa huduma ya WIKI au Tsh 1000/= kwa huduma ya mwezi” na kisha kujulishwa jinsi ya kusikiliza hadithi yake.

Kamando alisema huduma hiyo itamwezesha mteja wa Vodacom kujitoa muda wowote atakapojisikia na anaweza kurudi tena na kufurahia huduma ya Vodacom Hadithi pale atakapohitaji tena. Iwapo mteja atapata changamoto yoyote, atatuma neno MSAADA kwenda namba 15460 na tatizo lake litatatuliwa.

“Kuhusu kusitisha huduma hii, bw. Kamando alieleza kwamba mteja anayetaka kusitisha huduma, atatuma neno ONDOA au ACHA kwenda namba 15460 na huduma hii itasitishwa papo hapo.
“Vodacom inatoa OFA kwa wateja wake wa mwanzo ya kusikiliza hadithi za Shigongo bure kabisa kwa siku mbili za mwanzo,” alisema.

Na Mwandishi Wetu

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad