Wachezaji Lamine Moro, Kazimoto wafungiwa



BEKI wa kati wa Yanga, raia wa Ivory Coast, Lamine Moro, amefungiwa kucheza mechi tatu huku kiungo wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto akifungiwa michezo miwili kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya katika mchezo uliozikutanisha timu hizo Juni 17, mwaka huu.

 
Mbali na kusimamishwa kucheza, Lamine amepigwa faini ya Sh laki tano kutoka kwa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) ambao walitoa tamko lao hilo jana Alhamisi.Makosa hayo waliyafanya Jumatano ya wiki iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ambapo Lamine alimpiga teke Kazimoto dakika ya 85, lakini pia Kazimoto amefungiwa kutokana na kuanzisha vurugu uwanjani dakika ya 86, na wachezaji wote walionyeshwa kadi nyekundu.

Bodi ya Ligi imetoa taarifa hiyo kupitia barua ambayo imesainiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo

.Akizungumza na gazeti hili baadaye, Kasongo alifafanua kuwa, adhabu ya wachezaji hao imeanza kuhesabiwa tangu walipoanza kukosa michezo baada ya kupewa kadi nyekundu na ndivyo sheria inavyosema.

“Adhabu ya kukosa mechi imeanza kutekelezwa tangu walipopewa kadi nyekundu na siyo leo (jana) baada ya kutoa taarifa hizo, kwa sababu sheria inaonyesha kuwa, wachezaji wamezuiwa kucheza baadhi ya mechi, lakini katika utekelezaji wa adhabu tunaanza kuhesabu kuanzia mechi walizokosa baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu,” alisema Kasongo.

Hivyo, Lamine baada ya kukosa mchezo uliopita, pia atakosa dhidi ya Ndanda wikiendi hii, wakati Kazimoto amemaliza adhabu yake ya kukosa mechi mbili baada ya JKT Tanzania kucheza michezo miwili bila ushiriki wake
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad