Washauri wa Magufuli na Kisa Cha Mama Salma Kikwete



KATIKA makala iliyopita, nilizungumzia mambo yanayomsaidia Rais John Magufuli kufanikiwa katika utendaji na kuwa kiongozi bora duniani. Nilihoji nani washauri wake kwani anavyobuni mipango na mikakati ya kuendesha nchi, miradi ya kimkakati, kukuza uhusiano wa diplomasia na nchi za nje n.k inaonesha kuwa, ana washauri wazuri wenye uwezo mkubwa wa kazi hiyo.

Ni kama niliotea Rais Magufuli alikuwa mbioni kuwaonesha hadharani, baadhi ya washauri hao. Si wengine, bali marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, Dk Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne na mawaziri wakuu wastaafu. Waliofuatilia sherehe za uwekaji jiwe la msingi la ofisi mpya ya Ikulu, Dodoma watakubaliana nami kuwa, viongozi hao bado ni lulu kwa taifa.

Ndiyo maana haishangazi kila anapowaita kushiriki nao hafla ya kiserikali, huwaomba waseme kitu kwa wananchi kama ushauri wao. Kwa mfano, siku hiyo, Rais Mkapa baada ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimtaka aendelee kuchapa kazi zaidi.

“Mbele kwa mbele,” Rais Mkapa alimalizia kwa maneno hayo akizidi kumtia moyo Rais Magufuli kuendelea na kasi hiyo. Rais Mstaafu Kikwete akasema: “Well done, keep it up,” yaani, safi sana endelea hivyo hivyo. Hata Mzee Mwinyi alimsifu Rais Magufuli kwa mengi, zamani na sasa kujenga Ikulu, Dodoma.

Ujumbe wao ulikuwa ni kukubali kazi za JPM. Kwa wachambuzi wa siasa, kukubali kazi za JPM hadharani na hata wanapokutana naye faragha ina uzito mkubwa kwa wasiomkubali.

Kumkubali kwao kunaongeza uzito wa JPM kukubalika nao na wananchi kwa imani kuwa, kama anayofanya si mazuri, hata viongozi hao wenye uzoefu wa nafasi yake, wangemkosoa. Hii inatokana na historia ya Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Nyerere kusema wazi mambo aliyoamini hayaendi vizuri wakati wa awamu ya pili yaliyotishia uhai wa nchi wakati aliyapigania kufa kupona kwa maslahi yetu.

Mambo hayo ni nyufa za ukabila, udini, rushwa, tishio la viongozi kuvunja Muungano, kuzikwa kwa Azimio la Arusha lililokuwa msingi mkuu wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea sambamba na haki.

Katika mkutano na vyombo vya habari na wananchi, Nyerere aliwahi kusema asingekuwa tayari kuiona nchi ikisambaratika huku akiangalia tu. Ndiyo maana alikemea dalili za watu kujinadi kwa ukabila akidai makabila yalikufa na sasa yamebaki kwa ajili ya kutambika ma alikemea rushwa kiasi cha kumfanya Rais Mwinyi kuvunja serikali wakati huo.

Pia alikemea kuzikwa Azimio la Arusha akisema alilisoma kila mara na hakuona tatizo lake, alikemea viongozi wanaolilia kuvunja Muungano watakuta kuna Wazanzibari na Wazanzibara na hawatabaki salama na kujiapiza ikitokea hivyo, dhambi ya ubaguzi iwatafune. Ni ushauri ambao Mwalimu Nyerere aliutoa kwa Rais Mwinyi hadharani na umebaki kama rejea muhimu kwa siasa za nchi hadi leo hii.

Rais Magufuli alidhihirisha marais hao kweli ni washauri wake siku alipowaita wao na mawaziri wakuu wastaafu Ikulu, Dar es Salaam na kuteta nao masuala mbalimbali ili kuchota uzoefu wao. Hatua hiyo ilipongezwa na marais wa Namibia na Zimbabwe kuwa ni mfano wa kuigwa jinsi Tanzania inavyowaenzi viongozi wake wakuu wastaafu kwa kuwashirikisha kwa ushauri wao.

Na hicho ndicho kinachoipambanua Tanzania na nchi nyingine yakiwemo mataifa makubwa kama Marekani ambayo viongozi wastaafu wa Republican hawakumkubali Rais Donald Trump na hata wa chama cha upinzani, Democrat pia. Matokeo yake ni ghasia na vurugu, uporaji wa mali katika maduka na uchomaji moto ofisi kama hasira za Wamarekani weusi na wengine wanaoamini nchi inakosa uongozi thabiti baada ya tukio la kuuawa kinyama kwa George Floyd.

Mfumo wa Tanzania katika ushauri kwa Rais ni thabiti kwani ukiacha jopo la viongozi wastaafu hao, chama tawala, CCM kina Baraza la Wazee. Katika baraza hilo, wamo marais hao, viongozi wastaafu CCM, spika wa zamani, Pius Msekwa aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara na wengineo wanaoweza kumshauri Rais JPM ambaye sasa pia ndiye Mwenyekiti CCM.

Ni wazi kwa mfumo huo, huwezi kutarajia Rais makini, mwenye elimu ya kutosha ya ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) tena ya sayansi ya kemia, anaweza kushindwa kupanga mikakati ya kuongoza nchi vizuri zaidi.

Ndiyo maana haikushangaza aliposimama kidete kutoiweka nchi katika karantini kutokana na ugonjwa wa Covid-19 ulipoingia, akahimiza watu kuchapa kazi, kutumia tiba asili na kumwomba Mungu. Ukiacha wastaafu hao, Rais hupokea ushauri kwa wasaidizi wake wa fani za kisekta, sheria, diplomasia, ulinzi na usalama, siasa, uchumi, afya wanaopaswa kuwe na weledi mkubwa.

Hivi karibuni JPM amethibitisha anao baada ya kuwateua baadhi yao wakamsaidie kazi maeneo mengine ambapo aliyekuwa Mshauri wa Sheria kapelekwa kuwa Mkuu wa Wilaya Mtwara, wa uchumi akateuliwa kuwa Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa wa Pwani kuliko na viwanda vingi.

Aliyekuwa afya aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambako alithibitisha weledi kwani muda mfupi, alibaini madudu ya vifaa vibovu vya upimaji wa virusi vya corona na majibu feki ya vipimo. Liko pia Baraza la Ulinzi la Taifa ambalo Rais alionesha umuhimu wake majuzi jijini Dodoma aliposema ni moja ya taasisi alizoamua kuzihamishia huko mapema katika azima ya kuhakikisha serikali inahamisha makao makuu.

Umuhimu wa ulinzi na usalama wa nchi uko wazi kwa kila mtu, bila vitu hivyo, hakuna amani, hakuna uchumi na hivyo nchi itayumba ndiyo maana rais anahitaji ushauri makini. Ni kwa kujua hilo, JPM amekuwa makini kuteua wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama akitumia vigezo vya hali ya juu kuteua akisema hadharani sifa zinazofanya awateue kumsaidia.

Baadhi ya sifa ni uadilifu, uchapa kazi, ubunifu katika uongozi, weledi, ucha Mungu. Mfano alisema alimteua Brigedia Jenerali Suleiman Mzee kuwa Mkuu wa Jeshi la Magereza kwa sababu alijenga majengo ya kambi ya JWTZ kwa gharama nafuu kwa kutumia nguvu kazi ya askari na anatamani akaendeleze nidhamu hiyo magereza iliyoshindwa kujenga nyumba zake za askari hadi alipoagiza JKT wamalizie kazi hiyo. Kwa muktadha huo, ni wazi JPM anataka mtu mwenye ubunifu kama huo kuwa mshauri wake ndio maana naye anasisitiza matumizi mazuri ya fedha za serikali ili ziwe na tija zaidi.

Hata hivyo, ucha Mungu pia umekuwa kigezo kingine. Yeye ni mcha Mungu hivyo ni wazi anatamani washauri wake wawe wacha Mungu ndio maana haishangazi Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo ni ‘mtumishi’ wa Mungu pia.

Ndio maana sikushangaa pia siku Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Diwani Athumani (wakati huo akiwa bosi Takukuru) katika moja ya mabaraza ya Idd alipowaomba waumini wa Kiislamu wasaidie kupiga vita rushwa. Hata hivyo, si ucha Mungu tu.

Wote ni wachapa kazi; Jenerali Mabeyo alikisimamia kwa wiki nzima, kuopolewa kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Ukara. Hakupumzika hadi mwisho. Nilimfahamu Diwani kabla akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Shinyanga na Mbeya alikoacha historia ya kusafisha ujambazi akikaa ofisini hadi usiku kutoa maagizo ya kazi na baadaye Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Kuonesha Diwani alivyokuwa mchapakazi akiwa RPC Mbeya, nilifanya naye mahojiano usiku kuhusu usalama wa mkoa huo wakati naandaa dokumentari ya mafanikio ya Rais Kikwete ya ujenzi viwanja vya ndege nikiwa Ofisa Uhusiano/ Sheria Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) mwaka 2015.

Hii ilikuwa ni baada ya ratiba yake mchana kubanana zaidi ya mara mbili. Ndio maana Rais Magufuli alipomteua Diwani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kutoka Ukatibu Tawala wa Mkoa (RAS) Kagera, nilijua upele umepata mkunaji;

ushauri wake ni lulu. Kwa mafanikio ya miradi ya kimkakati; bwawa la umeme la Nyerere, ununuzi wa ndege nane mpya, utoaji elimu bure msingi na sekondari, ujenzi viwanda, reli ya kisasa SGR, viwanja vya ndege, ni wazi ana washauri wazuri wa uchumi.

Mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za majiji, wilaya, miji na taasisi na mashirika ya umma ni kati ya washauri wake pia wa sekta za kitaalamu walioko ‘site’ hivyo, mrejesho wao ni muhimu.

Ndiyo maana haishangazi ‘wasiotosha’ kwa uwezo wa kitaaluma, ubunifu, uadilifu na uchapakazi, amekuwa akiwatumbua tu na kuteua wengine. Taasisi nyingine za kumshauri ni Mahakama na Bunge mihimili ambayo maamuzi yake kukosoa au kuafiki ajenda za serikali ni ushauri tosha.

Mfano, uamuzi wa Mahakama kutupa madai ya mwanamke wa Tanga aliyelalamika mbele ya JPM siku ya Sheria, Dar es Salaam na Rais kuagiza asikilizwe, umekuwa kama ushauri wa kero kama hizo kusikilizwa na wahusika si rais. Ndiyo maana siku hizi ziarani wanapojitokeza kina mama wenye shida, JPM huagiza wakuu wa mikoa, wilaya wanaomsaidia wawasikilize.

Anasema si kila kero lazima aisikilize yeye. Ukiacha washauri hao rasmi, wako pia washauri wasio rasmi, vyombo vya habari vinaporipoti masuala yanayogusa wananchi na kumfanya ajue matatizo yao na kuagiza yafanyiwe kazi.

Kundi lingine ni la viongozi wa dini zote na hata machifu. Hawa humshauri pia na zaidi humwombea ulinzi wa Mungu, hekima, busara na salama aongoze nchi vizuri. Mwingine ni mkewe, Mama Janeth ambaye amejitoa kusikiliza shida za wazee na watoto yatima na kuwasaidia.

Kupitia kwake matatizo ya wazee humfikia pia JPM kwa utatuzi wake. Shuhuda wa nguvu ya mke katika siasa ni Rais Kikwete aliyekiri hakujua Mama Salma anajua siasa kiasi hicho hadi alipoonesha kipaji chake kumwombea kura za urais mwaka 2005 na 2010. Salma sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, jambo linaloonesha hata JPM anamkubali.

Hata hivyo, siasa za 50-50 zinaendelea kumbeba mwanamke labda awe na matatizo binafsi kama mke wa rais wa zamani Kenya ‘aliyepiga’ watu. Kwa washauri hawa rasmi na wa bure, vipi Rais mwenye uwezo mkubwa wa elimu, mchapakazi, mwadilifu, mcha Mungu, mpenda haki, anayependa watu wake, mzalendo kama JPM asipate mafanikio kama si hujuma? Tafakari.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad