Waziri Ummy Mwalimu "Kwa Kiasi Kikubwa Tumeithibiti Corona Tunaelekea Kuimaliza Kabisa"



Serikali imesema kuwa imefanikiwa kudhibiti na kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya virusi vya corona huku ikiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kuutokomeza kabisa.

Hayo yalisemwa leo na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa ziara yake ya kushtukiza kwenye kwenye Kituo cha Afya cha Ngamiani Jijini Tanga ambapo aliweza kuzungumza pia na wahudumu wa Afya na kupokea msaada wa vifaa vya kunawia maji kudhibiti Ugonjwa wa Covid 19 vilivyotolewa na Shirika la Water Mission Tanzania.



Mwalimu alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wananchi wake na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa imeweza kuudhibiti ugonjwa huo huku ikiendelea na juhudi za kuumaliza kabisa.

“Kwa kiasi kikubwa tumeweza kuidhibiti corona na sasa tunaelekea kuumaliza kabisa, tuachane na kusikiliza baadhi ya vyombo vya habari vya wenzetu wanaotaka kututisha kuhusu ugonjwa huu” Alisema.

“Lakini pia ndugu zangu waandishi wa habari mnaona hali halisi hapa tumefika hakuna mgonjwa hata mmoja wa corona, hivyo muwajulishe wananchi habari hizi kwamba ugonjwa tumeudhibiti na hatuna kituo chenye wagonjwa wa corona ndani ya mkoa wetu” Alisisitiza Mwalimu.



Aidha alifafanua kwamba wananchi wote wanaokwenda kupata huduma za kijamii ni lazima waendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya corona kwa kufuata maagizo ya serikali na wataalamu wa afya.

Awali alipofika katika kituo hicho cha afya alikuta hali ya msongamano wa wagonjwa katika eneo la kusubiria huduma ya kuonana na daktari.

Mwalimu alisema kuwa kutokana na msongamano huo kuna asilimia kubwa ya kupatikana maambukizi ya corona kwa wagonjwa hao ambao pamoja na kuvaa barakowa lakini walikaa kwa kubanana sana jambo ambalo limempa wasiwasi.

“Wagonjwa wamefuata tiba hapa lakini kuna wasiwasi watu wakaondoka na corona, mnatakiwa muendelee kujikinga, nimeona pale nje mnanawa kwa maji tiririka na sabuni, barakowa mmevaa lakini kwa mlivyokaa kwa msongamano mnaweza kuambukizana” alisema.


Hata hivyo waziri alimuagiza Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Ngamiani Angelina Mashaka pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji kupata eneo la kuongeza sehemu ya kukaa wagonjwa wanaofuata tiba ili kuepusha msongamano.

Vile vile alimtaka Mashaka kuendelea kuwakumbusha wagonjwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya corona wanapofika kupata tiba kwa kuzingatia tahadhari zote zinazotakiwa.


Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ummy Mwalimu kweli wewe kazi unaijua. Ubarikiwe sana.

    ReplyDelete
  2. Tumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote.

    Mh JPJM na wasaidizi wake naWananchi wote.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad