Waziri wa Kilimo Atangaza Mazao Yatakayouzwa Kwenye Mfumo Wa Stakabadhi Ghalani
0
June 01, 2020
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imetangaza rasmi mazao ya kuanzia yatakayouzwa kupitia mfumo maalumu wa uuzaji wa mazao wa Stakabadhi ghalani.
Mazao hayo ni pamoja na zao la Korosho ambalo limekuwa na mafanikio makubwa kupitia mfumo huo, mazao mengine ni Ufuta ambao utauzwa kwa mfumo huo katika baadhi ya maeneo nchini.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametangaza msimamo huo wa serikali wakati akizingumza ofisini kwake Jijini Dodoma juzi tarehe 30 Mei 2020 huku akiyataja mazao mengine yaliyoingizwa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na Choroko, Pamba, Dengu n.k pamoja na Kahawa itakayotumia mfumo huo kwa baadhi ya maeneo.
Waziri Hasunga amesema kuwa mfumo huo tangu umeanza kutekelezwa umekuwa na faida kubwa hususani katika mikoa ya kusini kupitia zao la korosho lakini umeleta changamoto kubwa katika maeneo ambayo misingi ya kuanzishwa kwa mfumo huo haijatimizwa.
Amesema kuwa ili mfumo wa Stakabadhi ghalani uweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa ni lazima kuwa na vyama vya Ushirika vya mazao vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe katika eneo husika.
Ameeleza kuwa lengo la kuwa na vyama hivyo ni kufanya kazi ya kukusanya mazao na kuyapeleka kwenye ghala kuu ambalo limesajiliwa na kuwa na viwango vinavyotakiwa.
Jambo jingine ni lazima kuwepo na muendesha ghala mwenye leseni anayetambuliwa na Bodi ya Maghala na lazima elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi ya namna ya kutumia mfumo huo na ushiriki wao katika kufuatilia minada itakavyokwenda.
Amesisitiza kuwa ili mfumo huo uweze kufanya kazi vizuri wanunuzi lazima wawepo, Mfumo utangazwe na kuuzwa hadharani kadhalika kuwe na mzigo wa kutosha pamoja na ubora wa uhifadhi ili kuwavutia wanunuzi.
Ameeleza kuwa sio mazao yote yanaweza kutumika katika mfumo wa stakabadhi ghalani ni baadhi ya mazao kulingana na uwezo wake wa kutunzwa na kukaa muda mrefu bila kuharibika. Hivyo kwa mazao ya mboga na matunda haiwezi kuwa jambo jepesi kuzitunza muda mrefu hivyo sio rahisi kuingia katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Ukichukua mazao kama karanga ukaweka kwenye mfumo huu, unaweza ukahifadhi lakini tatizo la karanga zinaweza zisiwe na unyevu unaokubalika hivyo kuna hatari ya kusababisha Sumu kuvu.
Waziri Hasunga amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani ilikuwa ni kulinda maslahi ya wakulima kwani mazao hukusanywa pamoja, kuwekwa kwenye madaraja kisha kupanga bei kwa pamoja hivyo kuuza kwa bei nzuri.
Mfumo huo unamuwezesha mkulima kupata mkopo popote baada ya kuwa na risiti ya stakabadhi ghalani wakati akisubiri mazao yake kuuzwa kwa bei nzuri
Kwa utaratibu mfumo wa stakabadhi ghalani unasimamamiwa na Bodi ya Maghala ambayo ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara hivyo kuikabili changamoto hiyo serikali imeihamishia Bodi hiyo wizara ya kilimo ili kupunguza muingiliano uliopo wa kimajukumu katika Wizara hizo mbili.
Mhe Hasunga amesema kuwa katika mikoa ambayo tayari vyama vya Ushirika vimeanzishwa mfumo huo unafanya vizuri lakini kwa mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Katavi ambapo vyama vya Ushirika havijaanzishwa mfumo huo hauwezi kufanya kazi.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb) ametoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo ambayo hakuna vyama vya Ushirika vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe, Hakuna maghala yaliyosajiliwa, na Hakuna wenye leseni wanaotambulika na Bodi ya Maghala kutowasumbua wananchi badala yake wauze kwa uhuru katika maeneo watakayo.
Kadhika, Waziri Hasunga amewataka wafanyabiashara watakaonunua mazao hayo kwa mzigo unaozidi Tani moja ni lazima Kodi za Halmashauri zilipwe kwa mujibu wa utaratibu wa kikanuni na kisheria.
Ameongeza kuwa moja ya majukumu ya wakuu wa Mikoa na Wilaya katika mfumo wa mazao ya Stakabadhi ghalani ni kusimamia biashara kwa kuzingatia taratibu bila wananchi kudhulumiwa ambapo wasimamizi ni vyama vya Ushirika, pamoja na Bodi ya Maghala
Tags