Rais wa zamani wa Sudan na wenzake 16 wanapandishwa kizimbani leo katika mahakama maalumu ya Khartoum kwa tuhuma za kufanya mapinduzi dhidi ya serikali iliyokuwa imechaguliwa na wananchi hapo mwaka 1989.
Kesi hii inatajwa kuwa ya kwanza ya aina yake na kwamba adhabu yake yumkini ikawa kifo.
Kesi hiyo imewasilishwa mahakama kwa mujibu wa kifungu nambari 96 cha sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 1983 ya Sudan na iwapo atapatikana na hatia yumkini akahukumiwa adhabu ya kifo.
Shirika la habari la FP limemnukuu mmoja kati ya wanachama wa timu ya mashtaka akisema kuwa, kuna ushahidi wa kutosha wa kumuweka hatia Omar al Bashir na wenzake.
Miongoni mwa shakhsia wakubwa wanaohukumiwa katika kesi hii ni pamoja na waliokuwa makamu wa rais wa Sudan, Ali Othman Taha na Bakri Hassan Saleh pamoja na wanajeshi na raia walioshika nyadhifa kadhaa za uwaziri na magavana wa majimbo tofauti ya Sudan wakati wa utawala wa al Abashir.
Mawakili 150 wanaomtetea Omar al Bashir wanasema kuwa, kesi hiyo inafanyika kwa malengo ya kisiasa.
Mapinduzi yaliyofanywa na Omar al Bashir mwaka 1989 nchini Sudan yalikuwa ya tatu tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1956 baada ya yale yaliyofanywa na Jeneral Ibrahim Abboud mwaka 1959 na Jaafar Nimeiry mwaka 1969