Balozi wa Urusi nchini Uingereza Andrei Kelin, amekanusha madai kwamba idara ya ujasusi nchini mwake ilijaribu kuiba taarifa kuhusu chanjo ya virusi vya corona.
Wakati wa mahojiano na shirika la habari la BBC kuhusu madai hayo yaliotolewa na Marekani, Uingereza na Canada wiki iliyopita, Kelin alisema kuwa hayana ukweli.Kelin aliongeza kuwa alifahamu kuhusu kuwepo kwa wadukuzi hao kutoka kwa shirika hilo la habari na kwamba katika ulimwengu wa sasa kuhusisha udukuzi wowote wa kompyuta na taifa lolote ni jambo lisilowezekana.
Siku ya Alhamisi, idara za kijasusi za Marekani, Uingereza na Canada zilishtumu kundi la udukuzi la APT29 linalojulikana kama Cozy Bear na linaloaminika kuwa sehemu ya idara ya ujasusi ya Urusi kwa kutumia programu ya kushambulia taasisi za utafiti wa elimu na dawa zinazohusika katika utengenezaji wa chanjo ya ugonjwa wa COVID-19. Haikubainishwa wazi iwapo habari zozote muhimu ziliibiwa.